Ubize wa wazazi, mmomonyoko wa maadili unavyowaweka watoto hatarini

“WAZAZI wengi tuko bize sana kutafuta fedha, hivyo hatushindi na watoto nyumbani na tukirudi tunakuta wamelala, tukiulizia tu wanaendeleaje basi na asubuhi tutatoka tena mapema,”haya ni maneno ya Jackline Massawe mfanyabiashara wa samaki.

Jack ni miongoni mwa wazazi wa Halmashauri ya Jiji la Ilala, mkoani Dar es Salaam, ambao wanawaweka watoto wao katika hatari ya kubakwa au kulawitiwa kutokana na kukosa ukaribu nao.

Sababu hiyo na nyingine zimekuwa zikichangia Ilala kuwa miongoni maeneo ambayo watoto wake wanakumbwa zaidi ya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji na ulawiti.

Mkoa wa Kipolisi  Ilala upo  katikati ya Jiji la Dar es Salaam, hili ni dhahiri kuwa huduma za kisheria ,usalama na elimu inapatikana kirahisi zaidi .

Licha ya urahisi huo Ilala  ni miongoni mwa mikoa ya jiji hilo ambayo matukio ya ukatili wa kingono  yanaongezeka ambapo  una matukio ya ukatili  292.

Katika  kituo cha Mkono kwa Mkono kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Amana,Wilaya ya Ilala inaripotiwa kuwa Watoto wawili hadi watatu wanafanyiwa vitendo vya kikatili kila siku.

Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii wa kituo hicho, Suphiani Mndolwa anasema ukatili unaoongoza kufanyiwa watoto ni ukatili wa kingono ambao ni ubakaji na ulawiti.

Mdolwa anasema ukatili huo mara nyingi unatokea ndani ya jamii, ambapo watoto wa kike ndio wanaoathirika zaidi.

Mndolwa anasema matukio hayo ya kikatili yanasababishwa na uangalizi mdogo wa watoto, momonyoko wa maadili, visasi na imani za kishirikina.

Anasema kwa kiasi kikubwa ukatili unasababishwa na wazazi kutokuzingatia au kufuatilia  malezi ,makuzi na maendeleo ya watoto.

Anasema katika kesi walizofatilia wapo watu ambao utotoni mwao walifanyiwa vitendo vya kikatili kama ulawiti na hivyo mioyo yao inabaki na visasi.

“Na kwa sababu wana visasi walipizia kwa watoto,wengine ni miili kuingia taamaa hivyo watu waliopitia ukatili wanahitaji kutibiwa kisaikolojia,”anasisitiza.

Anasema kuna watu wakati mwingine wazazi/walezi wanawafanyia ukatili watoto kutokana na imani za kishirikia eti watapata mali, kitu ambacho sio sahihi.

HALI ILIVYO

Utafiti uliofanywa na serikali  kwa kushirikiana na shirika la watoto ulimwengunia ( UNICEF) unaonesha asilimia 60 ya matukio yanatokea nyumbani na asilimia 40 yanatokea shuleni.

Takwimu za Polisi nchini zinaonesha katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2020 jumla ya makosa 11,001 yaliripotiwa ikilinganishwa na makosa 12,223 kwa mwaka 2019 hili ni ongezeko la matukio 190 sawa na asilimia 1.2.

Makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ya matukio ni kubaka (5,867), kumpa mimba mwanafunzi (3,631) na kulawiti (1,000).

Matukio ya kikatili yanaongezeka kila mwaka ambapo kwa mwaka 2016 kulikuwa na matukio 10,551,mwaka 2017 ni 13,457,mwaka 2018 ni 14,491,mwaka 2019 ni 15,680 na mwaka 2020 ni 15,870.

Katika Mkoa wa kipolisi wa Ilala matukio mwaka 2018 matukio ya kikatili yalikuwa 291,mwaka 2019 matukio yalikuwa 334 na mwaka 2020 matukio 292.

Jack anaeleza kuwa kubadilika kwa mfumo wa malezi ya watoto katika jamii  akijumuisha ubinafsi unachangia ubakaji na ulawiti.

“Unajua maisha yamebadilika sasa wazazi tuko bize kutafuta  na wazazi wanapokuwa hawapo watu waliowazunguka wale watoto wanaona kuwa sio wa kwao hivyo wanawafanyia ukatili,”anasisitiza Jack.

James Kamala anasema momonyoko wa maadili na imani za kishirikiana zinachangia watoto wengi kukumbwa na ukatili wa kingono hasa ubakaji na ulawiti.

“Kuna haja ya kurekebisha upya jamii tukianza na watoto katika suala zima la upendo na ushirikiano na wazazi tuache kuwa bize tuwape muda watoto, ili kama kuna viashiria vya ukatili wa kingono watueleze tujue mapema,”anashauri Kamala.

KUACHA  MILA NA DESTURI  INACHANGIA?

Katika Mahojiano Mwenyekiti  wa baraza la Ustawi wa Wazee  Mkoa wa Mbeya, Arthum Mwankenje anaeleza kuwa ukatili unatokana watu kuondokana  na utamaduni wa upendo, ambao kila mmoja alikuwa ndugu na kila mtoto alikuwa mtoto jamii nzima na  sasa imebaki mtoto ni wa mtu mmoja.

Mzee Mwankenje anasema Matokeo  ya hayo yote huruma kwa  mtu kwa mtoto asiye wake hakuna.

“La pili kumeingia mila potofu hasa biashara za kishirikina zimechangia kuleta vitu ambavyo havistahili watu wamemuacha Mungu,” anasema.

Kwa mujibu wa Mwankenja mambo kama  momonyoko wa maadili watu kuacha kupendana, kukosa huruma  na kusaidiana hakupo kabisa kila mmoja ni yeye tu.

“Hii imekwenda mbali  hata ndani ya familia upendo umeondoka  mfano Mtoto wa miaka mitatu anapelekwa nje ya nyumba anaenda kufundishwa, matokeo yake hata katika kukua mambo ya nyumbani hajui kwa sababu hajalelewa kijamii au kifamilia.

“Hapo kwanza wazazi tunaanza ukatili kwa watoto bila kujua huko nyuma haikwepo, lakini hata malezi ya msichana wa kazi sio malezi ya kifamili kwa hiyo vyote vimeondoa mamlaka na uwezo wa kumlea mtoto,” anasema.

Anasema matokeo ya hayo yote ni mtoto asiye wa kwako sio wa kwako na kukiuka msemo wa ‘mtoto wa mwezio ni wako’.

Anashauri jamii kurudi katika utamaduni wao kwa kushikamana ,kurudisha upendo na kurudi kwenye mamlaka ya kuwalea watoto katika maadili mema badala ya kulelewa na wengine.

“Tumeletewa mno vitu vya magharibi kiasi ambacho tunaona ni sahihi, kumbe sio kila kitu ni sahihi turudi kwetu,”anasisitiza.

VIONGOZI WA DINI WANENA

HabariLEO ilifanya mahojiano na viongozi mbambali wa dini ambao wameeleza sababu za matukio ya kikatili kwa watoto kuongezeka hasa ubakaji na ulawiti.

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Rukwa ,Ostazi Mohhamed Adam anasema vitendo hivyo vinatokana na mmomonyoko wa maadili unaoendelea kwa sasa.

Anafafanua kuwa wao wana jukumu la kuhakikisha na kuhamasisha malezi mazuri katika jamii na pale vinapojitokeza vitendo vya ubakaji na ulawiti wamekuwa wakichukua hatua madhubuti.

“Ikiwa ni pamoja na kushauri watu wanaofanyiwa vitendo hivyo kuwaelekeza kufika katika dawati la jinsi la Jeshi la Polisi, ambalo sasa wamekuwa wakisimamia na hatua stahiki zinachukuliwa

“Vitabu vya  dini vinaelekeza vizuri juu ya haki na malezi, lakini pia taratibu za maisha kwa maana  hivyo tunawashauri wazingatie misingi ya dini, uzuri dini zote zinaelekeza zimekuwa zikiwafundisha watu kuwa na hofu ya Mungu na kufuata maagizo ya Mwenyezi Mungu,” anasema.

Askofu  Emanuel Komba Kutoka Songea,Ruvuma, pia analilia kukosekana kwa maadili sahihi kuanzia kwenye familia mpaka kwenye masuala ya dini ndio chanzo cha ukatili

“Lazima jamii ielekezwe kwenye elimu kama madhehebu ya dini  watu wanavyohudhuria kanisani wanaamini kwamba vitu kama hivi ni dawa ya kujiepusha na vitendo hivi, lakini wengine  hawaendi kanisani na wengine wakajiingiza katika dawa za kulevya na maisha yasiyofaa yanahamasisha wawe na tabia za kikatili ,”anaeleza.

Anabainisha kuwa watu wanapokwenda makanisani wataelimishwa na kujengewa hofu ya Mungu na kujali utu, hivyo hawatathubutu kufanya ukatili.

 

MADHARA YA UKATILI KWA WATOTO

Msaikolojia tiba katika Hospitali ya Taifa Ya Muhimbili, Isack Lema anasema kuwa ukatili kwa mtoto una madhara makubwa ikiwemo madhara ya kisaikolojia na kimwili.

Anasema tafiti zinaonesha kuwa mtoto aliyefanyiwa ukatili kuna uwezekano mkubwa wa kuwafanyia ukatili watu wengine.

“Madhara ya ukatili ni makubwa, hivyo waathirika wanatakiwa kupatiwa matibabu sio ya kimwili tu hata kisaikolojia ili kumuweka sawa akaendelea na maisha yake mazuri,”anaeleza.

WAZAZI WATAKIWA KUFANYA HAYA

Tafiti zinaonesha kwamba watoto ambao hawajajengewa ukaribu na wazazi wao hukosa uwezo wa kujiamini na hivyo kushindwa kueleza masaibu yao kwa mtu yoyote na mara nyingi huwa waathirika wa ukatili.

Fatuma Kamramba  ni Meneja Huduma ya simu kwa watoto Zanzibar,  anaeleza mzazi anapaswa kuwa tayari muda wote kumsikiliza mtoto na ili hili litokee inabidi mzazi kuanza mapema kujenga ukaribu na mahusiano  mazuri yenye upendo na mwanae.

Kwa mujibu wa Fatuma  ni muhimu kuwa na uhusiano ambao utamfanya mtoto ajiamini na kwamba mama au baba ni kimbilio lake endapo ana jambo linamtatiza  na anataka kulitolea taarifa

Anamini kwamba wazazi ni kimbilio na msaada na wapo tayari kumsikiliza na kushughulika na taarifa zake kwa kumuamini.

“Kwanza kabisa mzazi akipata taarifa awe mpole na asimuoneshe mtoto kwamba kaogopa sana juu ya taarifa, ili kumpa mtoto nafasi ya kujieleza zaidi, amhakikishie kwamba amefanya vizuri kutoa taarifa  na kwamba kilichotokea sio makosa yake asimlaumu,”anasisitiza Fatuma.

Anasema katika hali hiyo mzazi aanze kumshauri mtoto kwa kuzungumza naye ili kujua kwa undani zaidi na amwambie hatua atakazochukua

”Kama mzazi ataona hawezi kuzungumza na mwanae hasa aliyefanyiwa ukatili wa kingono anaweza kuomba ushauri kwa mtaalamu au kupiga namba 116,” anasema.

Anasema watoto wanapaswa kulelewa kwa namna ya kujiamini  na kuwaheshimu wazazi badala ya kuwaogopa.

“Ukimjengea mwanao mazingira rafiki ya kukufikia na kuamini wewe ni msaada kwake, atakuwa huru kujieleza kwako hivyo nawashauri wazazi wajenge utaratibu wa kuzungumza na mtoto ,kuwapa taarifa muhimu za kutambua taarifa muhimu za kutambua viashiria vya udhalilishaji na namna ya kujilinda katika umri mdogo ili kuweza kuwalinda watoto dhidi ya ukatili hasa wa kingono,”anashauri.

Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Tumaini Mwenge, Cristian Bway anasema wazazi wengine hawana uelewa wa namna ya kushughulika na watoto wa kizazi cha sasa, kwani wanaishi kwenye mazingira ambayo wanapata taarifa nyingi na wanajifunza vingi huku wazazi wakiwa hawafatilii.

“Zamani mambo ya ndani kuhusu uzazi yalikuwa hayasemwi hii ni hatari na watoto hawana watu wa kuwaelekeza njia nzuri, hivyo wakikutana na watu wabaya wanafayiwa na hawaelewi kama ni kitu kibaya,” anasema.

Bway ambaye pia ni mwanasaikolojia anasema sasa kuna tatizo la wazazi kuwa karibu na watoto na kuwajengea kujiamini, hivyo anapokutana na kitu cha kumhatarisha hawawezi kusema kwa sababu anaogopa.

Anasema Kuna haja ya kujenga ukaribu kati ya mzazi na mtoto

“Zamani baba akienda kutafuta mama yuko nyumbani na ndio mlezi hivyo uwezekano wa mtoto kukutana na watu wa hatari ulikuwa mdogo sasa wazazi wana mambo mengi, baba anatoka na mama anatoka mtoto hana wa kumuangalia hilo linachangia sana,”anabainisha Bway.

Anasema ni muhimu wazazi kupata muda wa kukaa na watoto na kuzungumza nao ili kutengeneza mazingira ya kujiamini .

JITIHADA ZA SERIKALI

Wazira wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum  Dk Dorothy Gwajima anabainisha kuwa, pamoja na jitihada mbalimbali za kukabiliana na vitendo vya ukatili, bado taarifa za vitendo hivyo hususani kwa watoto zinaendelea kuongezeka ikiwemo ubakaji, ulawiti, utumikishwaji wa watoto katika ajira hatarishi, ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni na vitendo vingine vya ukatili.

“Wizara kwa kushirikiana na wadau wake tunaratibu kampeni shirikishi ya jamii inayoenda kwa jina la SMAUJATA (Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii, 2022). “

Dk Gwajima pia anatoa wito kwa wazazi na walezi  kuzingatia kuwa karibu na watoto ,kuwafundisha kutokubali mtu kugusa mwili wake na kutopokea zawadi zozote.

“Ulinzi wa mtoto unaanza na ukaribu wa mzazi na mtoto wake ,natoa wito kwa wananchi wote kujiunga na kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na ustawi wa Jamii(SMAUJATA) ili kuongeza nguvu ya kupaza sauti,”anasisitiza Dk Gwajima.

Habari Zifananazo

Back to top button