Uboreshaji Bandari Tanga kukamilika 2023

UTEKELEZAJI wa mradi wa kuboresha Bandari ya Tanga unatarajia kukamilika Aprili mwaka 2023.

Meneja wa bandari hiyo, Masoud Mrisha amesema wakati wa ziara ya waandishi wa habari wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini waliotembelea bandari hiyo leo.

Amesema mradi   huo wenye thamani ya Sh bilioni 429.1 ulianza kutekelezwa mwaka 2019 na sasa umekamilika kwa asilimia 83.

Amesema mradi huo ulikuwa na utekelezaji awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza imekamilika.

“Mradi huu ulikuwa unatekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza imeshakamilika,” amesema na kuongeza kuwa awamu ya pili itakamilika na kukabidhiwa mradi Aprili mwaka 2023.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha (katikati) akizungumza leo. (Picha zote na Anne Robi, Tanga).

Kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha bandari hiyo kuwa na uwezo wa kuhudumia shehena tani 3,000,000 kutoka tani 750,000 kwa sasa.

Mrisha amesema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji ilikuwa ni kuongeza kina cha maji (draft) kutoka mita 3 hadi 13 na upana wa mita 73 kwenye njia ya kuingizia na kutokea meli kutoka mita 3 hadi Mita 13 yenye kipenyo cha Mita 800.

Kwa awamu ya pili, Meneja huyo amesema mradi ulilenga kuboresha magati mawili yenye urefu wa mita 450.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button