Ubunifu waipaisha kamati usalama barabarani

KITENGO cha Usalama Barabarani nchini kimetangaza kuguswa na ubunifu wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa kikisema unakiongezea kitengo chao kasi katika kukabiliana na makosa mbalimbali ya barabarani.

Msimamizi na Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani (CTMC) nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Frasser Kashai ametaja ubunifu wa kamati hiyo kuwa ni pamoja na mgao wa fedha za stika za usalama barabarani kutumika kununua magari kwa ajili ya kikosi cha barabarani cha mkoa huo.

“Ubunifu mwingine ni huu uliotangazwa sana na vyombo vya habari hivi karibuni wa kufunga kamera katika barabara tata ili zisaidie kuwanasa madereva wanaokiuka sheria za barabarani,” alisema DCP Kashai.

Aliyasema hayo katika ziara yake na maafisa wengine wa kitengo chake iliyofanyika mkoani Iringa ili kujionea mafanikio na changamoto za Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa katika kutekeleza shughuli zake.

Kashai alisema kama ilivyotokea kwa mikoa mengine kuiga ubunifu wa kamati ya Iringa kununua magari ya kwa kutumia fedha za stika, hakuna shaka kwamba hata suala la kufunga kamera katika maeneo hatari kwa ajali litaigwa na mikoa hiyo.

“Tunaipongeza sana kamati ya Iringa na tunaiomba iendelee kubuni na kukisaidia kikosi cha usalama barabarani kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, DCP Mstaafu Mohamed Mpinga alisema dhamira ya kamati hiyo katika kukabiliana na usalama barabarani ni kubwa na akaitaka ifikirie pia namna ya kubuni vyanzo vya mapato vitakavyosaidia kwa haraka utekelezaji wa mipango yao.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Asas alisema uamuzi wao wa kutumia fedha za stika kununua magari, umekiwezesha kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Iringa mpaka sasa kupata magari manne likiwemo moja la kubeba wagonjwa au majeruhi.

“Tutaendelea na mpango wa kutumia fedha za stika kununua magari ili kukiwezesha kikosi chetu cha usalama barabarani kufika katika maeneo mengi yanayohitaji huduma yao,” Asas alisema.

Kuhusu kamera za barabarani, Asas alisema; “Kwa kuanzia kamati yangu inajitolea kufunga kamera hizo katika maeneo hatarishi zaidi ambayo ni pamoja na eneo la Majinja Mafinga na Mlima Kitonga wilayani Kilolo.”

Alisema kwa kupitia kamera hizo, kikosi cha usalama kitaweza kufuatilia mienendo ya madereva na kuona matukio yanayohusu uvunjaji wa sheria kupitia maafisa wake waliopo ofisini na kuwasiliana na askari waliopo jirani ili wachukue hatua.

“Tunaamini mpango huu ukifanikiwa, utakuwa mpango wa nchi nzima na utasaidia sana kudhibiti au kumaliza ajali katika maeneo mengi nchini,” alisema.

Kuhusu vyanzo vya mapato, Asas alisema kamati yao inacho kiwanja katika eneo la Gangilonga mjini Iringa kitakachotumiwa kwa uwekezaji pindi taratibu zitakapokamilika.

Wakati huo huo Asas amezitilia shaka takwimu za ajali katika maeneo mbalimbali mkoani Iringa akisema nyingi kati ya zinazotokea hasa katika maeneo ya vijijini haziripotiwi.

“Kuna jambo lazima lifanyike ili kuwezesha taarifa za ajali zote zinazotokea kuhakikisha zinafika Polisi na kufanyiwa kazi,” alisema.

Awali Katibu wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wa mkoa huo, Mosi Ndozero alitoa taarifa ya kamati ya mkoa na maazimio mbalimbali yaliyofikiwa na kamati hiyo katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za usalama barabarani.

Pamoja na taarifa hizo, Ndozero aliomba nyongeza ya askari wa usalama barabarani mkoani kwake akisema idadi waliyonayo ni ndogo ikilinganishwa na jiografia ya mkoa huo.

Habari Zifananazo

6 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button