Uchimbaji visima Nzuguni kupunguza tatizo la maji

TATIZO la maji katika Jiji la Dodoma litapungua baada ya uchimbaji wa visima Nzuguni kukamilika mapema mwakani ambavyo vitaongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 50.8 ya sasa hadi asilimia 75.

Akielezea mkakati wa mkoa kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) kwa wafanyabiashara na walipakodi mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema mipango ya upatikanaji wa maji inaendelea vema.

“Kukamilika kwa visima katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma kutaongeza kiwango cha upatikanaji maji kutoka asilimia 50.8 ya sasa hadi asilimia 75,” alisema.

Senyamule alisema, mkakati wa mkoa katika kupunguza tatizo la maji ambayo kadiri ya mipango ya awali kabla ya serikali kuhamia Dodoma maji yaliyokuwapo yangetosha hadi mwaka 2030.

Kutokana na kuongezeka kwa watu na watumishi, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2022 idadi ya watu katika Mkoa wa Dodoma imeongezeka kutoka milioni 2.085 ya mwaka 2012 hadi milioni 3.085, ongezeko hilo limekuja na upungufu wa huduma mbalimbali ikiwemo ya maji.

Senyamule alisema kwa kujua hilo kwamba kuna ongezeko la watu, serikali imeweka mikakati ya kutatua changamoto hiyo ya maji kwa njia ya dharura ya kupata maji haraka kutoka kwenye visima vya Nzuguni. Mradi wa visima vya Nzuguni unaendelea kutekelezwa kwa haraka, ukikamilika mapema mwakani utaongeza upatikana wa maji katika Jiji la Dodoma katika maeneo hayo na maeneo jirani.

Senyamule alisema mkakati mwingine ni kutumia maji yanayopatikana katika Bwawa la Zuzu lililopo katika Kata ya Zuzu ambalo maji yake yataelekezwa Nala ambako kumetengwa kwa ajili ya uwekezaji mbalimbali ukiwemo ujenzi wa viwanda.

Katika mkakati wa muda wa kati, utafiti unafanyika ili kuona kama itawezekana kuvuta maji kutoka katika Bwawa la Mtera ili kuongeza kiwango cha maji katika jiji hilo.

Utafiti huo ukikamilika na kubaini kwamba inawezekana kuvuta maji kutoka katika bwawa hilo, ndani ya miaka miwili serikali itatekeleza mradi huo ili kupunguza kama si kuondoa kabisa changamoto ya maji katika Jiji la Dodoma.

Katika mkakati wa muda mrefu, Senyamule alisema ni kuvuta maji kutoka katika Bwawa la Falkwa, katika Wilaya ya Chemba. Bwawa la Falkwa likitengenezwa kwa kujenga kingo za maji katika milima inayozunguka eneo hilo yatapatikana maji ya kutosha.

Mradi huo wa miaka sita, ukianza na kukamilika utaleta suluhisho la kudumu katika Jiji la Dodoma ambalo kwa sasa lina changamoto kubwa ya maji.

Mkakati mwingine wa muda mrefu ni kuvuta maji kutoka katika Ziwa Victoria ambayo kwa sasa tayari yamefika katika Wilaya ya Igunga katika Mkoa wa Tabora, baadaye yatafika katika Mkoa wa Singida na kuvutwa hadi katika Jiji la Dodoma.

Mradi huo unaotazamiwa kukamilika ndani ya miaka 10, utamaliza kabisa tatizo la maji katika jiji hilo ambalo linakua kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa watumishi, wananchi pamoja na wawekezaji.

Mkuu wa Mkoa alisema wawekezaji wanatakiwa kufika Dodoma kuwekeza kwani ni mahali sahihi kuwekeza, kwani changamoto chache zilizopo ikiwemo ya upungufu maji mkakati umewekwa kuzimaliza.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x