TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inachunguza mchakato wa uhamishaji wa wananchi kutoka Hifadhi ya eneo la Ngorongoro kuhamia kwenye Kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga
Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro amesema leo Aprili 25, 2023 Bungeni mjini Dodoma kuwa uchunguzi huo, Tume ilitembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kijiji cha Msomera mkoani Tanga, na kupata maelezo ya wananchi.
Aidha, Tume ilikutana na mamlaka mbalimbali za Serikali na baadhi ya Asasi za Kiraia (AZAKI) kwa ajili ya kupata maelezo zaidi.
Amesema, lengo la uchunguzi huo ni kubaini iwapo kulikuwa na uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika zoezi hilo la wananchi kuhamia Kijijini Msomera kutokea Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ili hatimaye kuweza kutoa mapendekezo kwenye mamlaka husika.
Amesema, taarifa ya uchunguzi huo inaendelea kuandaliwa na ikikamilika itawasilishwa kwenye mamlaka husika.