DAR ES SALAAM: MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umepanga kufikisha mawasiliano kwenye maeneo matano zikiwamo barabara kuu, maziwa, mbuga, visiwa na hifadhi za taifa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa wahariri na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mashiba alisema wakati mfuko huo unaanzishwa mwaka 2009, ulilenga kufikisha mawasiliano katika maeneo zaidi ya makazi ya watu ikiwemo vijijini ambako huduma ya mawasiliano ilikuwa asilimia 45 lakini sasa imefikia asilimia 96.
“Mradi wetu mkubwa utakuwa ni kuhakikisha njia zote kuu za barabara zinapata mawasiliano ili kuongeza usalama kwa watumiaji. Lakini pia tunalenga maeneo kama vile maziwa, mbuga, visiwa na hifadhi za taifa,” alisema.
Mashiba alisema kwa upande wa maziwa kwa kushirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC), wanatarajia kujenga minara mitano ikiwamo mitatu ya Tasac na UCSAF itajenga miwili.
Aliomba wadau likiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), kushirikiana na mfuko huo kufikisha mawasiliano katika maeneo ya hifadhi kwa kuwa ni muhimu kwa usalama wa watumiaji wa maeneo hayo.
Mashiba alisema pia UCSAF inatekeleza mradi wa tiba mtandao kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na hospitali saba zimeunganishwa ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Rufaa Morogoro.
“Kupitia tiba mtandao daktari wa Muhimbili anaweza kumtibia mgonjwa aliyeko Geita,” alisema.
Mashiba alisema kwa sasa huduma hiyo inakamilishwa kuunganishwa pia katika hospitali za mikoa ya Ruvuma, Tanga, Katavi, Nzega na Chato.
Alisema kwa Zanzibar zinaunganisha hospitali ya Abdala Mzee iliyopo Pemba na Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja iliyopo Unguja ambapo utekelezaji wake upo katika hatua za mwisho.
Mashiba alisema zaidi ya Watanzania milioni 23.7 wanatarajia kupata huduma ya mawasiliano ya simu ya uhakika, baada ya mfuko huo kuingia mikataba na watoa huduma wa mawasiliano ya kufikisha huduma hiyo katika kata 1,974 zenye vijiji 5,111 kwa kujenga minara 2,149.
Alisema hadi sasa kata 1,197 zenye vijiji 3,613 na wakazi takribani 14,572,644 wameshafikishiwa huduma ya mawasiliano, baada ya minara 1,321 kujengwa katika kata hizo.
“Utekelezaji pia unaendelea katika kata 777 zenye minara 828, vijiji 1,498 na wakazi 9,226,204, huku gharama (ruzuku) za utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni Sh bilioni 326,” alisema Mashiba.
Kuhusu hali ya mawasiliano nchini, alisema shule 1,120 zimefikishiwa vifaa vya Tehama kwa wastani shule kupewa kompyuta tano, printa moja na projekta moja.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2022/23 shule 150 zilifikishiwa vifaa vya Tehama, huku bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 ikiwa ni Sh bilioni 1.8.
Mashiba alisema UCSAF inatarajia kufikisha huduma ya mtandao wa intaneti katika vituo vya magari ya mwendokasi awamu ya kwanza na pili, na mazungumzo na watoa huduma bado yanaendelea.
Kuhusu kuongeza uwezo wa minara, alisema mfuko huo umeingia makubaliano na watoa huduma kuongezea nguvu minara 127 na hadi kufikia Novemba 20, 2023, minara 111 tayari imeshaongezewa nguvu kutoka kwa watoa huduma, gharama za mradi huo ni Sh bilioni 5.14 utekelezaji wa maeneo yaliyobakiwa yanatarajiwa kumalizika ifikapo Desemba.
Kuhusu mradi wa Tanzania ya kidijiti, Mashiba alisema minara 758 itajengwa katika kata 713, mikoa 26 na wilaya 127 itanufaika pindi mradi huo ukikamilika, Watanzania milioni 8.5 watanufaika na mradi.