TAASISI isiyo ya kiserikali ya Usevya Development Society (UDESO) mkoani Katavi, imeelezea mafanikio ya mradi wa ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za umma (PETS), ikiwa ni pamoja na baadhi ya changamoto zilizobainika katika sekta ya afya kuanza kufanyiwa kazi.
Akizungumzia mafanikio ya utafiti uliofanywa na Kamati ya Ufuatiliaji Matumizi ya Rasilimali za Umma, Mratibu wa mradi huo Paul Masanja, amesema ni pamoja na baadhi ya ajenda zilizoibuliwa na kamati ikiwemo malalamiko ya wananchi kuhusu upatikanaji wa dawa katika zahanati na vituo vya afya.
Amesema ilibainika kuwa tatizo sio la wahudumu bali ni kutokana na mlolongo wa upatikanaji wa dawa hadi kufika kwenye vituo kutoka bohari kuu ya dawa.
Amesema, tatizo la baadhi ya wahudumu wa afya kutovaa sare wanapokuwa maeneo ya kazi pia limeanza kufanyiwa kazi, ikwemo vichomea taka.
Naye Ofisa Mipango Msaidizi Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Benjamin Richard amesema mradi huo licha ya kuwa umetekelezwa kwa kipindi kifupi, lakini umewakumbusha ofisi yao katika ufuatiliaji wa miradi na utumiaji wa rasilimali hasa fedha katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi (UDESO), Eden Wayimba, ametoa rai kwa jamii kuthamini miradi inayotekelezwa na serikali na kuhakikisha majengo yanayojengwa hayachakai.
Februari 19, 2023 kamati ilikabidhi ripoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga, ambapo moja ya changamoto zilizobainishwa ni mazingira ya kutolea huduma katika zahanati na vituo mbalimbali vya afya kutokuwa rafiki.
Changamoto nyingine ni upungufu wa vitendea kazi katika Zahanati ya Mbede, ukosefu wa uzio katika Zahanati ya Mbede na Kibaoni hali inayosababisha watoto kuingia kirahisi kuokota makopo ya dawa na mifugo kukatiza.
Hata hivyo, baada ya kuipokea ripoti hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga aliipongeza taasisi ya UDESO kwa kutoa ripoti hiyo kwa kile alichodai itaisaidia serikali kujua wapi kuna changamoto na kufanyia kazi upungufu uliobainishwa, ili kuongeza ufanisi zaidi.