DAR ES SALAAM; CHUO Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kimesema kina mpango wa kutafuta wadau na wabia watakaotengeneza tibalishe, ili watu wazipate katika maeneo mbalimbali na kutumia katika kuepusha magonjwa yasiyoambukiza.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Lugano Kusiluka amesema hayo Dar es Salaam katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayoendelea.
Amesema UDOM ni chuo cha kwanza kutoa cheti Cha shahada ya lishebora, hivyo wana watalaamu ambao wako tayari kutengeneza lishe, kwani vyakula vingine ni tiba.
SOMA:https://habarileo.co.tz/udom-watafiti-tiba-upungufu-wa-damu/
Amesema kupitia mpango huo pia wanawakaribisha wajasiriamali, ili kushirikiana nao katika kutengeneza tibalishe, jambo litakalowezesha taifa kuwa na watu wenye afya bora.
” Katika Chuo hiki tunafundisha wataalamu katika nyanja mbalimbali na kwenye eneo la tibalishe kutasaidia kupunguza wimbi la magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yamekuwa yakiibuka kwa kasi,” amesema.
Kuhusu ubunifu amesema lengo la chuo hicho ni kuanzisha kongani, ili waweze kukuza ubunifu walio nao na pia kutengeneza bidhaa kwa ubora zaidi na Watanzania wote waweze kuzitumia.