UDOM waandaa mitaala ufugaji nyuki, samaki
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kinaandaa mitaala ya muda mfupi kwa ajili ya wananchi kupata elimu juu ya ufugaji nyuki, ufugaji samaki na kilimo cha bustani.
Akizungumza kwenye viwanja vya maonesho ya wakulima Nanenane Nzuguni jijini Dodoma, Mhadhiri kutoka Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati, Dk Faith Mpondo, amesema kuwa wanaanzisha kozi hiyo fupi ili kuwapa wananchi kujifunza na kupata utaalamu mbalimbali.
“Tunaandaa mitaala ya muda mfupi kwa ajili ya wananchi kupata elimu, kozi hizo fupi zitakuwa hazina masharti yoyote ,” amesema.
Dk Mpondo amesema kuwa Idara ya baiolojia wana siku maalum kila mwaka ambayo hufanyika mwezi Juni, wananchi hufika kujifunza wanapatiwa taarifa mbalimbali.
Amesema kuwa katika ndaki ya sayansi asilia na hisabati kumekuwa na mafunzo mbalimbali kwa vitendo yanayotolewa kwa wanafunzi ili wanapomaliza chuo waweze kujiajiri .
“Tuna mizinga ya nyuki, mabwawa ya samaki na kilimocha bustani, wanafunzi wanapata ujuzi mkubwa na hata wengine wanaibua bunifu zao mbalimbali,” amesema
Amesema kuwa uzalishaji wa mazao ya nyuki ni fursa nzuri katika kuongeza kipato. Amesema kuwa wamekuwa wakirina asali kupitia mizinga na kisha makapi ya asali hutumika kwa ajili ya kutengeneza nta na nta wamekuwa wakitumia kutengeneza mishumaa, mafuta na bidhaa nyingine.