UDSM kusaidia elimu shule maalumu Sinza

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeingia makubaliano na Shule Maalumu Sinza kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalumu wanapata elimu inayohitajika.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye alisema watafanya kila linalowezekana kuhakikisha walimu wao wanafanya kazi hiyo nyeti kwa mafanikio na ufanisi mkubwa.

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, alimtaka Mkuu wa Shule Kuu ya Elimu chuoni hapo, Dk Eugenia Kafanabo kuandaa makubaliano ya mpango huo.

Advertisement

“Nimemuagiza mkuu wa shule yetu kuu ya elimu aandae MoU (makubaliano) ili hawa watoto na walimu wao wasikwame katika utoaji huduma,” alisema na kuongeza kuwa makubaliano hayo yataainisha maeneo ambayo wataweza kusaidia.

Alisema chuo hicho kinaendelea kufanya shughuli mbalimbali katika jamii ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya miaka 60 ya chuo hicho.

“Chuo chetu kina majukumu makuu matatu ambayo ni kufundisha, kufanya utafiti na kuhudumia jamii. Sasa leo tumefika hapa kutekeleza takwa la tatu la kurudisha kwa jamii na tumewaletea vitu mbalimbali vya kusaidia watoto hawa maalumu,” alisema.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kiti mwendo, vifaa vya burudani, televisheni, ving’amuzi, vifaa vya michezo na vya shule vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 10.2.

Mkuu wa Shule Kuu ya Elimu wa chuo hicho, Dk Kafanabo alisema makubaliano hayo yataainisha mahitaji mbalimbali ikiwamo walimu.

“Hapa chuoni tunafundisha na tuna wakufunzi wa watu wenye mahitaji maalumu kama hawa watoto, hivyo kama watahitaji walimu tutawapatia maana wapo wengi wenye fani hiyo. Sasa hii MoU itaweka wazi mambo yote tutakayowasaidia,” alisema.

Mwalimu Mkuu wa Shule Maalumu ya Sinza, Catherine Msese alishukuru kwa msaada huo wa vifaa walivyovipata ambavyo vitawasaidia watoto hao katika masomo mbalimbali.

“Tunawashukuru UDSM kwa msaada wao mfano hicho kiti kitatusaidia sana badala ya kuwabeba watoto mgongoni, sasa watakuwa wakitumia wheelchair,” alisema.

Alisema watoto hao wanajifunza zaidi kwa kuona hivyo watakavyokuwa wakiendelea kuangalia michezo mbalimbali kwenye televisheni, itawasaidia kujua mbinu mbalimbali ili nao waweze kushiriki kwenye mashindano.

Alisema shule inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za walimu wenye taaluma ya kufundisha watoto wenye uhitaji maalumu.