UDSM wabuni mbinu usagaji viungo

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imetengeneza teknolojia rahisi ya kuwawezesha vijana na wanawake kusaga viungo mbalimbali vikiwemo mdalasini, iliki, pilipili manga na vinginevyo ambavyo hutumiwa kwa matumizi ya nyumbani.

Mwanafunzi wa mwaka wa nne chuoni hapo anayesomea Uhandisi wa Kilimo pamoja na Mitambo, Gloria Mshana ameeleza hayo katika maonesho ya Kimataifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

Amesema mashine hiyo ina uwezo wa kusaga kilo moja kwa dakika moja au kwa maana nyingine inasaga kilo 60 kwa saa moja.

“Tumebuni mashine hii baada ya kuangalia soko la viungo tumeona wakulima wanalima viungo lakini unakuta wanawauzia madalali ambao wanavipeleka sokoni kuviuza.

“Tukaona kwa nini mkulima asivitengeneze mwenyewe viungo hivyo kisha kuviuza sokoni? Ili kumrahisishia mkulima tukaja na mashine hii ya kusaidia wakulima wadogo wadogo,” amesema.

Amesema katika kubuni mashine hiyo pia wamewaangalia vijana wajasiriamali kama wanaweza wakaunga kikundi kisha wakawa na mashine hiyo wakanunua viungo na kuvisaga kisha kuviingiza sokoni vitaboresha maisha yao.

Alisema mashine hiyo kwa kuwa ni teknolojia rahisi na gharama yake ni ndogo, itasaidia kutoa tatizo la ajira kwa vijana na wanawake kwa kuwawezesha kununua viungo, kuvitengeneza, kuviwekea nembo kisha kuviuza.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko chuoni hapo, Dk Dotto Kuhenga amesema chuo hicho katika maonesho hayo ya wakulima, wafugaji na wavuvi wana huduma za kitaalam zinazohusiana na kilimo, uvuvi, sayansi za bahari na ufugaji.

“Wataalam wameleta vitu mbalimbali pia wana utaalamu wa udongo wa kisasa uliotengenezewa rutuba ambao mtu anaweza kufanya kilimo cha mjini,” amesema.

Ameshauri wanaoishi mijini kujifunza kuhusu udongo huo, pamoja na mashine za kisasa zinazochakata korosho pamoja na viungo mbalimbali.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button