UDSM waja kivingine zaidi

DAR ES SALAAM; WANATAAALUMA 268 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM), wameanza masomo katika robo ya pili ya mwaka 2023/ 2024.

Kati ya wanataaluma hao, 49 wanasomea shahada ya umahiri na 219 shahada ya uzamivu, ambayo ni sawa na asilimia 67 ya wanataaluma wote 398 walioko masomoni kwa sasa.

Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, eneo la utafiti, Profesa Nelson Boniface amesema hayo alipokuwa akielezea nafasi ya chuo hicho katika tathmini ya utendaji wa vyuo vikuu duniani.

Profesa Boniface amesema jitihada hizo zinafanywa na serikali kwa kushirikiana na chuo hicho, lengo likiwa ni kupandisha hadhi chuo hicho kitaifa, kikanda na kimataifa.

“Kigezo cha idadi na ubora wa wanataaluma ndio nguzo kuu ya kufanya vizuri. Hivyo basi UDSM imejikita zaidi katika kuwekeza katika idadi na ubora wa rasilimali watu, ili kupandisha hadhi chuo kitaifa, kikanda na kimataifa,” amesema.

Mkakati mwingine alioutaja ni kuimarisha utafiti kwa kuwekeza Sh bilioni 10.5 kwa miaka mitano mfululizo kutokana na fedha zinazotokana na vyanzo vya ndani.

Vilevile kuanzishwa kwa ofisi ya kuratibu ushirikiano na tasnia mbalimbali, sera mpya ya majarida na kudhibiti ubora wa machapisho.

Amesema chuo hicho kimekuwa kikishiriki katika mchakato wa upimaji wa viwango vya vyuo vikuu duniani unaofanywa na taasisi mbalimbali au makundi ya watu.

“Ushiriki huu wa moja kwa moja ni uthibitisho wa ukomavu wa chuo kudhihirisha ubora wake katika utoaji wa elimu ya juu, utafiti na utoaji wa huduma za ushauri kwa umma,” amesema.

Pia amesema matokeo ya upimaji wa vyuo vikuu kutoka kwa mawakala au vikundi tofauti, yamekuwa yakitofautiana na kukosa uwiano kutokana na kila mmoja kuwa na vigezo tofauti.

 

Habari Zifananazo

Back to top button