UDSM wajivunia kutoa vijana wanaoweza kujiajiri

UDSM wajivunia kutoa vijana wanaoweza kujiajiri

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kupitia Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( CoICT), kimesema mbinu na maarifa mbalimbali wanayotoa kwa wanafunzi wao, zimewezesha wahitimu waliomaliza chuoni hapo kujiajiri na kuweza kuajiriwa.

Rasi wa Ndaki ya Tehama chuoni hapo, Profesa Joel Mtebe, amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya miaka 60 ya chuo hicho yanayoendelea pamoja na miaka 10 ya Ndaki hiyo.

Profesa Mtebe amesema kupitia fani hiyo ya Tehama, wameweza kuwasaidia vijana wengi kuwa na shughuli ya kufanya, kwa sababu tehama ni kitu tofauti kidogo na fani nyingine.

Advertisement

Amesema Ndaki hiyo imetatua changamoto ya ajira nchini ndani ya miaka 10 iliyopita.

Pia amesema wahitimu mbalimbali kutoka CoICT, wamehusika kwenye mabadiliko ya kidijitali  ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Amesema ndani ya miaka 10 hiyo wametoka wataalam wabobezi wanaochangia ukuaji na matumizi ya tehama.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Dk Leonad Binamungu, amesema maadhimisho hayo yatafanyika Septemba 23 mwaka huu.

Amesema Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Gabari, Kundo Mathew anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.