Uelewa wa tabianchi bado changamoto

UTAFITI uliofanywa umeonesha kuwa wananchi hawana uelewa wa kutosha katika suala la mabadiliko ya tabianchi, hivyo ipo haja ya kuandaa miradi mbalimbali itakayoongeza uelewa zaidi.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (Repoa), Dereck Msafiri amesema hayo wakati akitoa taarifa ya matokeo yaliyopatikana kuhusu uchafuzi na utunzaji wa mazingira.

Msafiri amesema pamoja na kutoelewa mabadiliko ya tabianchi, wananchi wametaka kuhusishwa katika utatuzi wake ikiwa ni pamoja na kuhusisha serikali za mitaa.

“Kwenye tabianchi uelewa bado ni mdogo, kwa hiyo katika suala la kisera kuna haja ya kuandaa miradi mbalimbali, ambayo mwisho wa siku inaweza kuongeza uelewa wa suala la tabianchi, kwa sababu watu wakipewa uelewa itarahisisha kupunguza athari za tabianchi katika nchi yetu,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti wa Repoa, Lucas Katera ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji, Dk Donald Mmari amesema utafiti huo ulifanyika kwa lengo la kuangalia mazingira na tabianchi kwa sababu ni mada muhimu katika mijadala mbalimbali ya maendeleo kitaifa na kimataifa.

“Utafiti umeangalia uelewa wa watu kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi, lakini pia kuangalia ni nani anapaswa katika kupambana na athari hizo,” amesema.

Amesema jambo hilo lina umuhimu katika utungaji wa sera, kwani tabianchi ni changamoto kubwa inayoikumba dunia kwa sasa, hivyo ni vizuri wananchi wakaelewa.

“Suala la sera ni vizuri kuliangalia ili kwamba uelewa ukiwa mdogo athari zinaweza kuwa kubwa, kwa sababu hawajui ni nini wafanye kwa hiyo ni muhimu kuangalia katika masuala ya wananchi kuelewa maana ya tabia nchi,” amesema.

Kwa upande wake mtaalamu wa mazingira, Fadhila Hemed amesema ripoti hiyo imetoa mwelekeo wa jumla wa mambo ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Habari Zifananazo

Back to top button