Uendelezaji wa fukwe eneo lenye kukuza uchumi

TANZANIA imejaliwa kuwa na vyanzo vingi vya maji, kama vile bahari, maziwa na mito, ni nchi iliyo na fukwe za kuvutia zaidi na za kipekee.

Fukwe hizo zina uwezo mkubwa wa kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi.

Kama maliasili, fukwe huongeza uzuri wa pwani, kutoa makazi kwa viumbe, wakiwemo ndege na kasa.

Advertisement

Kiuchumi, fukwe zinazosimamiwa vizuri hutoa fursa kwa ukuaji wa utalii ambapo nchi inapata mapato kutokana na watalii wa ndani na nje wanaotembelea maeneo ya pwani.

Akizungumza hivi karibuni katika Jukwaa la Maendeleo Endelevu, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo anasema uendelezaji wa fukwe ni jambo muhimu na nchi nyingi zilizowekeza humo zimepata maendeleo makubwa.

Katika jukwaa hilo, wadau wamekutana kujadili usimamizi madhubuti wa fukwe kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Singo anasema zipo fursa kadha wa kadha ambazo wawekezaji hawajazifikia na kwamba suala la utalii ni eneo linalohitaji kupewa kipaumbele.

Utalii kando ya fukwe huwezesha ukuaji wa shughuli za biashara, hasa hoteli na maduka makubwa, masoko ya kitamaduni na michezo, shughuli ambazo zinaweza kukuza nafasi za umma zinazojumuisha.

Kwa mfano, nchini Afrika Kusini maendeleo ya ufukwe wa V&A Waterfront uliopo Cape Town imechangia takribani Rand bilioni 223.7 (sawa na Dola za Marekani bilioni 15.46) kwa Pato la Taifa kufikia 2017, na iliongeza nafasi za kazi 36,163 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja na kuvutia zaidi ya watalii milioni 23.1.

Aidha, anasema hali hiyo ipo pia katika fukwe za Durban, Sfax, Tunisia, Dubai, na Dakar nchini Senegal.

Hata hivyo, maeneo ya fukwe nchini Tanzania hayajaendelezwa licha ya kuwa na uwezo mkubwa. Anasema wanakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii, kiuchumi na kimazingira.

Kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kama vile uchimbaji haramu wa mchanga, utupaji taka ngumu na oevu, ujenzi holela na uvuvi wa baruti unatawala kwenye fukwe mbalimbali.

Kutokana na ongezeko la watu na shinikizo kwenye rasilimali za Pwani, upo mmomonyoko wa fukwe na kiwango cha uharibifu mikoa ya Kanda ya Pwani kama Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Lindi na Pwani.

“Matumizi yasiyodhibitiwa ya misitu na mikoko hutokea kila siku,” anasema Kadari na kuongeza kuwa ni vyema kutambua kwamba, bila hatua zinazofaa za usimamizi na mipango mizuri ya uwekezaji, maeneo ya fukwe ya kuvutia yanaweza kuharibiwa kabisa na/au kumezwa na maji hadi mwisho wa karne ya 21.

Mambo yanayochangia uendelevu dhaifu wa maeneo ya fukwe na usimamizi wa rasilimali za pwani nchini ni pamoja na miundombinu duni, athari za hali ya hewa mabadiliko katika ukanda wa pwani na ukosefu wa wataalamu wabobevu nchini wa kuendeleza maeneo hayo ya fukwe.

Pia ukosefu wa sera na mipango inayoeleweka ya muda mrefu kuhusu uwekezaji na usimamizi wa maeneo ya fukwe.

Iwapo serikali haitachukua hatua za haraka katika kuwekeza na kusimamia fukwe zake, hatari ya majanga ya kibinadamu na ya asili itaongezeka.

Akizindua jukwaa hilo jijini Mwanza, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameagiza uongozi wa kila mkoa wenye fukwe kuharakisha kuandaa mpango mkakati wa namna ya kuendeleza maeneo ya fukwe ili yaongeze utalii na kukuza uchumi nchini.

Dk Mpango aliwakaribisha wawekezaji katika maeneo ya fukwe na kutumia fursa zilizopo kwa kuwa hazijatumika kikamilifu kwa maendeleo nchini.

Alisema Tanzania ni nchi ya kipekee yenye maziwa, bahari na hata mito kwa wingi, ikiwa na kilometa 1,400 za ukanda wa Pwani ya bahari, hifadhi tatu za bahari na maeneo tengefu 15 ya bahari ambayo hayajatumika ipasavyo.

Alisema fukwe hazijaendelezwa zimekuwa sehemu ya kuongeza uharibifu wa mazingira, zikikabiliwa pia na uchimbaji wa mchanga, kutupwa kwa taka maji na hata ujenzi holela, kilimo na ufugaji holela na athari zake kuonekana kwenye fukwe.

Dk Mpango aliagiza kila mkoa ukishirikiana na Ofisi ya Rais Mazingira kuharakisha kuandaa mpango mkakati na kila mkoa kufanya jambo litakaloongeza utalii.

Naibu Waziri Maliasili na Utalii, Mary Masanja anasema asilimia kubwa ya fukwe zinamilikiwa na watu binafsi na viongozi wa mitaa. Alisema ipo haja ya kuangalia upya sheria ya umilikishaji wa maeneo ya fukwe ili kuwa na utalii wa fukwe kwa maendeleo endelevu.

Mwakilishi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Neema Mwakatobe, alishauri serikali kushirikisha wananchi kuanzia ngazi ya chini inatekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo inayofanyika kwenye fukwe kuondoa manung’uniko.

Anasema wananchi wasiachwe nyuma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na wajulishwe pia ni ipi iliyotengwa kwa ajili yao ili watakapokuwa wakitakiwa kupisha eneo linalotakiwa wasibaki kulalama na kuona hawakushirikishwa.

“Lengo ni wawezeshwe kushiriki katika ukuaji wa uchumi nchini, wajue fursa zipi zimetengwa kwa ajili yao na wasibakie kuwa sehemu ya kikwazo katika mradi,” anasema Mwakatobe.

Haiwezekani mradi utekelezwe, wananchi washirikishwe lakini kiuchumi wabakie palepale…inahitajika uwezeshaji wa ziada kuhakikisha wanapiga hatua,” anasema Mwakatobe na kuongeza kuwa kama mwananchi alikuwa akitandaza dagaa asibakie hapohapo bali mradi uoneshe kumkuza kiuchumi.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwezeshaji nchini (EPZA), Innocent Umbulla anashauri serikali za mitaa na za mikoa zichukue jukumu la kuweka mbele uwekezaji wa miundombinu wezeshi kama barabara na umeme katika maeneo ya miradi ya uwekezaji.

Kadhalika waainishe vivutio vya uwekezaji vilivyopo katika eneo husika ikiwa ni pamoja na maeneo ya fukwe.