Ufadhili Costech watengeneza ajira 300

UFADHILI wa Serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) wa Sh milioni 32 kwa mbunifu wa mtambo wa kuchakata zao la mchikichi Dar es Salaam, umewezesha kupatikana kwa zaidi ya ajira 300.

Mbunifu huyo George Buchafwe ameeleza hayo wakati timu ya waandishi wa habari na maofisa kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), walipotembelea mtambo huo uliopo eneo la Viwanda Vidogo vidogo (Sido), Ving’ung’uti Dar es Salaam.

Buchafwe amesema fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya kutengeneza mtambo huo uliofanyiwa ubunifu wa kutengeneza mafuta lishe, mafuta ya kujipaka, sabuni za kufulia na kuogea.

“Kutokana na mtambo huu tumeweza kuajiri watanzania zaidi ya 300 ambao wanafanya shughuli tofauti tofauti ikiwemo kuchakata mafuta ya mawese ya njano, kupata mafuta mekundu ambayo yana faida katika mwili wa binadamu kwa kuwa na vitamin A, D, E na K, sabuni za miche za kufulia, za kuongea,” amesema.

Pia amesema waliweza kubuni mashine nyingine ambazo zimefungwa nje ya Mkoa wa Dar es Salaam, ambako wakulima wa chikichi zaidi ya 150 wanapata huduma ya kuchakata.

Amesema kupitia ubunifu wa mitambo hiyo, mnufaika wa kwanza ni wakulima wa chikichi, kisha kwa wale wengine wanaokuwepo kiwandani kwa ajili ya kuchambua makapi, mbegu nzima na zile zilizovunjika.

Pia kupitia Costech ambapo walimpa ufadhili huo waliweza kutoa elimu kwa wananchi, mpaka sasa wana viwanda vidogo 105 vilivyotokana na ufadhili huo.

“Kati ya viwanda hivyo 105 kila kiwanda kimoja kinaajiri watu saba ajira ya moja kwa moja lakini kinaajiri watu 120 ajira isiyokuwa ya moja kwa moja,” amesema.

Msimamizi wa kiwanda cha kusindika mawese kilichopo Mkuranga Pwani, Pascal Mhina amesema zaidi ya wanawake 20 kila siku wanafika katika kiwanda hicho na kuchambua mbegu za chikichi kuzitenganisha makapi, zilizo nzima na zilizovunjika.

Mnufaika wa mradi huo ambaye anafanya kazi ya kuchambua mawese yaliyosindikwa, Mariam Ramadhani amesema ajira hiyo kwa uchache inamwezesha kuendesha maisha yake.

Naye Meneja Uhifadhi Taarifa na Machapisho katika tume hiyo, Dk Philbert Luhunga amesema, ziara hiyo ya Costech inalenga kuonyesha jinsi fedha zinazotolewa na serikali kupitia tume hiyo zinavyotoa matokeo chanya kwa jamii.

Habari Zifananazo

Back to top button