Ufalme wa Simba SC Afrika ni suala muda tu

TIMU ya Simba imemaliza safari yake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kutolewa katika hatua ya robo fainali na mabingwa watetezi, Wydad CA ya Morocco wiki iliyopita.

Hii ni mara ya nne sasa kwenye misimu mitano, Simba inatolewa katika hatua hiyo hiyo kwenye michuano ya klabu Afrika na kushindwa kukata kiu ya mashabiki zake na Watanzania wanaopenda soka.

Wadau wengi wanaamini huu ulikuwa ndio wakati sahihi Simba kufanya hivyo na kuonesha umwamba wake zaidi ya hapo baada ya kuonesha kuwa ni kitu cha kawaida sasa Wekundu hao kufika robo fainali.

Presha imekuwa kubwa kwa Simba kuhusiana na kutocheza hatua ya nusu fainali ingawa imekuwa ikizimwa na kiwango kikubwa cha upambanaji wao kwenye mechi za robo fainali.

Inaaminika kwa ukubwa wa umri wa Simba wa miaka 87, umaarufu wao Afrika, mtaji wa mashabiki ilionao ilistahili kufanya jambo kwenye michuano hii mpaka sasa hata kwa kufika fainali.

Pia uwekezaji uliofanywa na bilionea Mohamed Dewji kwenye klabu hiyo unachagiza kuiweka Simba kwenye mizani ya kupambana na matajiri wengine wakubwa Afrika. Hata hivyo, pamoja na yote,

Simba inastahili pongezi baada ya kukosolewa mno kuhusiana na kushindwa kwao kutinga nusu fainali kila msimu. Naipongeza Simba kwa ujasiri wao wa kuwa na mfululizo wa kufika hatua hiyo.

Kwanza imetengeneza hadhi yake kwamba ni lazima ifike hapo kila msimu kisha mambo mengine ndiyo yatajulikana. Kwa bahati mbaya, ufalme wa mchezo wa soka upo kama ujenzi wa Mji wa Roma, haukufanikiwa au kuibuka tu baada ya siku moja, ni suala la muda, uvumilivu, uwekezaji wa akili na nguvu pia.

Hakuna timu inayotaka kwenda kushinda vita bila ya kufahamu uchungu, maumivu, mateso, mahangaiko, njaa na kila aina ya adha ya vita hiyo kabla ya kufanikiwa kuuona ushindi baadaye. Ukiona kwenye mapambano unafanikiwa tu bila ya vikwazo ujue kuna shida kubwa sehemu ambayo siku ukiigundua itakutesa mno na inaweza ikakuweka chini kwa muda mrefu sana.

Nachelea kusema Lunyasi wapo katikati ya vita, wameshaona utamu na adha ya kupambana na wapinzani wanaowazidi maarifa sehemu kadhaa na wanachopaswa kufanya ni kuendelea kufurahia mateso yao sasa dhidi ya wapinzani ili baadaye wavune faraja. IMEONJA LADHA ZOTE Ndiyo, Simba imetolewa mara nne kwa vipigo tofauti na timu kutoka nchi tofauti.

Simba iliondolewa mara ya kwanza kwenye robo na TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasi ya Congo. Mazembe kutoka Afrika ya Kati iliilazimisha suluhu Simba kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kisha ikaenda kuishindilia Simba mabao 4-1 Uwanja wa Mazembe, Lubumbashi.

Mara ya pili Simba ikiwa ugenini Afrika Kusini ikachapwa na Kazier Chiefs mabao 4-0 na kwenye mechi ya marudiano Simba ikashindwa kuupanda mlima wa mabao hayo na kuishia kuifunga Kaizer mabao 3-0 pale kwa Mkapa.

Msimu uliopita, Simba ilidondokea michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilipofika robo ikakutana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambapo kila timu ilishinda bao 1-0 nyumbani kwake kabla ya Simba kufungwa kwa panelti 4-3.

Msimu huu wamekutana na mabingwa watetezi, Wydad ambao nao wameitoa Simba kwa penalti 4-3. Kwa mantiki hiyo, Simba imeshaonja kila ladha ya kipigo lakini kilichotoa faraja ni namna robo yao ya mwisho walivyopambana na bingwa mtetezi ambaye kufika nusu fainali sio ishu kwake, ilivyohakikisha haitolewi kama ilivyotolewa na Mazembe na Kaizer huko nyuma.

HATUA NI KUBWA Wengi wanaona kama vile Simba inafeli kuishia robo kila msimu lakini nyuma ya pazia imepiga hatua kubwa sana kwa namna ilivyopambana na Wydad na kuipa joto la mechi kweli ya kibingwa. Sasa hivi Simba haitaki tena kutolewa kirahisi, ni aidha itakufunga kwake kisha ukaizidi kete kwako na mwisho hatua ya matuta ichukue nafasi yake, hatua ambayo haina mwenyewe na haijawahi kuwa na mwenyewe.

Ukiachana na hayo, Simba kwa sasa inafahamu silaha zinazotumika na timu za Afrika Kaskazini, Afrika ya Kati na Afrika Kusini kwenye hatua ya mtoano ya michuano hiyo hivyo ikirejea itakuwa na silaha ya ziada kwenye vita ya msimu ujao. Unaweza kusadiki kuhusu hatua hizi za Simba kama tu utarejea nyuma misimu michache iliyopita namna ilivyokuwa ikitapatapa kuingia makundi, kupambana kuvuka hatua ya makundi na sasa imekuwa mzoefu wa kuingia robo fainali. Ni hatua nyingi ndani ya misimu michache.

MFANO BORA TANZANIA Hatua za Simba haziishii kwao wenyewe tu bali hata kwenye kutengeneza njia ya timu nyingine Tanzania kufuata nyuma kwenye michuano ya klabu Afrika. Sizungumzii pointi ilizokusanya kwa ushiriki wake na kuiongezea pointi Tanzania, kuingiza timu nne kila msimu kwa sasa kwenye michuano hiyo ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) lakini namna ilivyosaidia kuongeza morali na hasira kwa timu nyingine nchini.

Yanga imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa ndiyo timu ya pili Tanzania kwa hivi karibuni kufika mbali katika michuano hiyo. Na tukubali kutokukubaliana kuwa ndani ya mafanikio hayo ya Yanga kuna hasira za maneno yanayosemwa kimyakimya ‘imekuwaje Simba inatuacha namna hii, inabidi na sisi tuoneshe kitu!’ Maneno ya namna hiyo sasa yapo kwenye vichwa vya viongozi wa timu za juu za Ligi Kuu Bara, zinawaza ubingwa, zinawaza michuano ya kimataifa, zinawaza uwekezaji mkubwa na kufahamika mno kisoka kama ilivyo Simba. Simba imefikia pakubwa kwenye mapambano yake, imebakisha hatua chache ngumu kudhihirisha umwamba wake. Kwa mtaji wa vipigo ilivyonavyo na ujanja iliovuna nyuma ya matokeo hayo hakika ina hazina kubwa ya ramani iliyojaa vichochoro vingi vya kuelekea kwenye mafanikio. Kilichobaki ni kuongezwa kwa umakini, juhudi, kupewa sapoti na kushikilia maradufu msimamo wa kiu ya mafanikio walionao kwenye soka la Afrika kisha tuache kudra na wakati ufanye kazi yake inayostahili.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button