UFARANSA inakusudia kupiga marufuku wanafunzi kuvaa ‘Abaya’ vazi lisilobana lenye urefu linalovaliwa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu katika shule za serikali. Waziri wa elimu wa nchi hiyo amesema kabla ya muhula mpya wa masomo.
Ufaransa imepiga marufuku alama za kidini katika shule za serikali tangu sheria za karne ya 19, baada ya kuondoa ushawishi wa kitamaduni wa Kikatoliki. Shule za umma Ufaransa haziruhusu uvaaji wa misalaba, kippa za Kiyahudi au hijabu za Kiislamu.
Mnamo mwaka wa 2004 nchi hiyo ilipiga marufuku hijabu shuleni, na mwaka 2010 ilipitisha marufuku ya nikabu na kuleta taharuki kwa Waislamu wa taifa hilo.
“Nimeamua kwamba abaya haiwezi kuvaliwa tena shuleni,” Waziri wa Elimu Gabriel Attal alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha TF1.
“Unapoingia darasani, hupaswi kuwa na uwezo wa kutambua dini ya wanafunzi kwa kuwatazama tu.
”
Hatua hiyo imekuja baada ya miezi kadhaa ya mjadala kuhusu uvaaji wa abaya katika shule za Ufaransa, ambapo wanawake wamepigwa marufuku kwa muda mrefu kuvaa hijabu.