Ufaransa yasafishwa tuhuma mauaji ya kimbari Rwanda

Ufaransa yasafishwa tuhuma mauaji ya kimbari Rwanda

MAJAJI wa Ufaransa wametupilia mbali kesi dhidi ya wanajeshi walinda amani wa Ufaransa waliotumwa wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.

Wanajeshi hao walinda amani walituhumiwa kuwa na mchango katika mauaji hayo.

Baadhi ya watu walionusurika katika mauaji hayo ya Juni 1994 katika vilima vya huko Bisesero Magharibi mwa Rwanda waliwashutumu wanajeshi wa Ufaransa kwa kuwatelekeza kwa makusudi kwa Wahutu wenye msimamo mkali waliowaua mamia ya watu katika eneo hilo ndani ya siku chache.

Advertisement

Baada ya malalamiko yaliyowasilishwa na walionusurika na mashirika ya kutetea haki za binadamu, waendesha mashtaka wa Ufaransa walianzisha uchunguzi Desemba 2005 mintarafu uwezekano wa kuhusika kwa wanajeshi hao katika uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Katika ripoti ya karibu kurasa 1,000, tume hiyo iliyoongozwa na mwanahistoria Mfaransa, Vincent Duclert, imetupilia mbali kesi dhidi ya wanajeshi wa Ufaransa kuhusika katika mauaji ya halaiki.

Majaji waliosimamia shauri hilo, wameamua kutoendelea na kesi dhidi ya wanajeshi hao wa Ufaransa, uamuzi ambao hata hivyo ulitarajiwa na wengi.

Wachunguzi hao hawakuweza kuthibitisha ushiriki wa moja kwa moja wa vikosi vya Ufaransa katika uhalifu uliofanywa katika kambi za wakimbizi na wala hawakubaini ushiriki kupitia misaada au usaidizi kwa vikosi vilivyohusika na mauaji ya halaiki.

Ufaransa, ambayo ilikuwa na uhusiano wa karibu na serikali ya kabila la Wahutu iliyokuwa madarakani wakati huo, ilipeleka maelfu ya wanajeshi nchini Rwanda katika ujumbe wa kulinda amani ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa wakati wa mauaji ya kimbari.

Karibu watu 50,000 waliuawa katika eneo la Bisesero lililoonekana kuwa kimbilio na ngome ya Watutsi waliojaribu kujilinda.

Ziara ya Rais Emmanuel Macron mjini Kigali mwezi Mei, 2021, iliashiria kurejea kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Ufaransa na Rwanda baada ya miongo kadhaa ya mivutano inayohusishwa na mauaji ya kimbari.