BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA), limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne kwa mwaka 2022 ambayo pamoja na ufaulu kuongezeka watahiniwa hawakufanya vizuri katika masomo ya sanaa na sayansi hasa somo la hisabati.
Watahiniwa 520,558 wa shule walifanya mtihani huo wa hisabati wa kidato cha nne kwa mwaka 2022 na kati yao waliopata daraja F ni 415,844 sawa na asilimia 79.92 ya watahiniwa wote.
Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Athuman Amasi alisema katika somo hilo watahiniwa 11,245 sawa na asilimia 2.16 ndio waliopata daraja A, watahiniwa 9,984 sawa na asilimia 1.92 daraja B, 4,783 sawa na asilimia 6.68 daraja C na 48,476 sawa na asilimia 9.32 walipata daraja D.
Amasi aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa katika mtihani huo takwimu zinaonesha katika somo la baiolojia watahiniwa 167,353 sawa na asilimia 32.16 walipata daraja F, watahiniwa 162,896 sawa na asilimia 31.30 walipata daraja D, 134,555 sawa na asilimia 25.86 daraja C, 34,077 sawa na asilimia 6.55 daraja B na 21,518 sawa na asilimia 4.13 walipata daraja A.
Alisema katika somo la fizikia, watahiniwa 36,135 sawa na asilimia 31.66 walipata daraja F, 47,140 sawa na asilimia 41.30 daraja D, 27,330 sawa na asilimia 23.94 daraja C, 3,009 sawa na asilimia 2.64 daraja B na 530 sawa na asilimia 0.46 ndio waliopata daraja A.
Alisema katika somo la kemia watahiniwa 10,816 sawa na asilimia 6.98 wamepata daraja A, 22,347 sawa na asilimia 14.42 daraja B, watahiniwa 72,565 sawa na asilimia 46.81 daraja C, 38,487 asilimia 25,47 daraja D na 9,792 sawa na asilimia 6.32 wamepara daraja F.
Amasi alisema hata katika masomo ya Sanaa bado watahiniwa hao hawakufanya vizuri na takwimu zinaonesha katika somo la uraia watahiniwa 155,891 sawa na asilimia 29.96 walipata daraja F na 3,982 sawa na asilimia 0.77 ndio waliopata daraja A.
Watahiniwa 18,506 sawa na asilimia 3.56 wamepata daraja B, 141,151 sawa na asilimia 27.12 wamepata daraja C na watahiniwa 200,863 sawa na asilimia 38.60 wamepata daraja D.
Masomo mengine ambayo wanafunzi hao hawakufanya vizuri ni historia ambapo watahaniwa 8,473 sawa na asilimia 1.66 tu ndio walipata daaraja A na 193,483 sawa na asilimia 37.99 daraja F na jiografia watahiniwa 3,236 sawa na asilimia 0.62 wamepata daraja A na 179,057 sawa na asilimia 33.90 wamepata daraja F.
Katika somo la kiingereza watahiniwa hao hawakufanya vizuri pia kwa kuwa 162,804 sawa na asilimia 31 wamepata daraja F na 115,297 sawa na asilimia 22.15 wamepata daraja C wakati somo la Kiswahili wengi wamefanya vizuri watahiniwa 71,745 sawa na asilimia 13.78 wamepata daraja B na 113,131 sawa na asilimia 7.4 wamepata daraja D na kiingereza
Kwa ujumla matokeo hayo yanaonesha watahiniwa wa shule 456,975 kati ya watahiniwa 520,558 wenye matokeo ambao ni sawa na 87.7 wamefaulu kwa kupata madaraja kuanzia daraja la kwanza, daraja la pili, daraja la tatu na daraja la nne.
“Kati yao Wasichana 243,285 sawa na asilimia 87.08 na Wavulana ni 213,690 sawa na asilimia 88.60. Ufaulu huu umeongezeka kwa asilimia 0.49 ikilinganishwa na mwaka 2021,” alisema Amasi.
Alisema katika eneo la ubora wa ufaulu waliopata kuanzia daraja la kwanza, la pili hadi la tatu kwa watahiniwa wa shule jumla ya watahiniwa 192,348 sawa na asilimia 36.95 walipata ufaulu mzuri wakiwemo wasichana 87,098 sawa na asilimia 31.18 na wavulana 105,259 sawa na asilimia 43.64 ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.11 ikilinganishwa na mwaka 2021.
Kwa upande wa mtihani wa maarifa (QT) alisema takwimu za matokeo zinaonesha watahiniwa 4,059 sawa na asilimia 42 ya watahiniwa 9,557 waliofanya mtihani wamefaulu. Mwaka 2021 watahiniwa 4,763 sawa na asilimia 57.23 walifaulu mtihani huo.
Aidha, Amasi alisema baraza hilo limefuta matokeo ya watahiniwa 333 kati ya hayo moja ni la mtahiniwa wa maarifa baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika mtihani na limefuta matokeo ya watahiniwa wanne walioandika lugha ya matusi katika skripti zao.
Pia, alisema NECTA imezuia matokeo ya watahiniwa 286 waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani huo na wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakufanya.
Amasi alisema watahiniwa 566, 636 walisajiliwa kufanya mtihani huo wakiwemo wasichana 306, 052 sawa na asilimia 54.01 na wavulana 260, 584 sawa sawa na asilimia 45.99 ya watahiniwa wote. Kati ya hao 534,753 walikuwa ni wa shule na 31,883 wa kujitegemea.