MRADI wa ufugaji samaki wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, umefanikiwa kuzalisha ajira 729, baada ya wananchi kupewa mafunzo ya kuendeleza ujuzi yanayotolewa kupitia ruzuku ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF).
Pia uzalishaji wa samaki umeongezeka hadi kufikia kilo 600 kwa miezi tisa kutoka kilo 100 za awali.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), imesema Mkurugenzi wa Kampuni ya RiverBanks Fish Farms, Pius Nyambacha, alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya mafunzo ya kuendeleza ujuzi kuhusu ufugaji wa samaki kwa wawakilishi kutoka Benki ya Dunia (WB), ambao ni wafadhili wa SDF.
Kwa maelezo ya taarifa hiyo, kupitia ruzuku ya mafunzo hayo, Kampuni ya RiverBanks Fish Farms imepata ufadhili wa Sh milioni 131.2 kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya ujuzi kuhusu ufugaji wa samaki.
Fedha hizo zimesaidia kuboresha miundombinu ya uzalishaji vifaranga vya samaki na kufugia, kuboresha na kujenga ofisi, kununua vifaa vya kisasa vya ufugaji pamoja na kuendesha mafunzo kwa vijana na kina mama 400 kutoka katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Rungwe.
“Lengo lilikuwa ni kutoa mafunzo na elimu kuhusu ufugaji samaki kwa watu 400, lakini kutokana na muitikio kuwa mkubwa, tulifanikiwa kufundisha watu 427 kwa kipindi cha miezi mitatu,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye amesema lengo la mfuko huo ni kuwezesha vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.