Ufuta waongeza ajira nchini

UONGEZWAJI wa thamani katika zao la ufuta umewezesha kutoa ajira mbalimbali kwa vijana na wanawake hapa nchini ikiwemo kutengeneza mafuta ya ngozi.

Mafuta hayo ya ngozi yanapunguza fangasi na bakteria kwa kuwa ndani ya ufuta kuna kemikali na virutubisho mbalimbali pamoja na vitamin E.

Mratibu wa Program ya Ufuta Kitaifa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Naliendele kilichopo Mtwara Joseph Nzunda amesema hayo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

“Mafuta haya yanaitwa Sesalemo yanatokana na ufuta pamoja na kwamba yana mchanganyiko wa vitu vingine lakini asilimia 90 zaidi inakua ni ufuta,”amesema.

Amesema kama kauli mbiu ya maonesho haya kwa mwaka huu inavyosema,’Vijana na Wanawake ni msingi Imara wa Mifumo endelevu ya Chakula,’ imekwenda na uhalisia kwa kuwa vijana na wanawake ni watumiaji wa zao hilo katika kuongeza mnyororo wa thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Ametaja bidhaa nyingine zinazotokana na zao hilo kuwa ni mafuta ya kula, siagi, kashata, unga, mashudu ya mifugo kama kuku, mbuzi na wengineo.

Amesema bidhaa mbalimbali zikiongezwa thamani kupitia zao hilo, ufuta utatumika zaidi hapa nchini pamoja na kwamba kwa asilimia 93 ni zao la biashara linapelekwa nje ya nchi.

Habari Zifananazo

Back to top button