RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (Fufa), Moses Magogo amesema timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ itajiondoa kwenye michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) itakayofanyika mwakani kutokana na hali mbaya ya kifedha.
Magogo amelazimika kuzungumza hayo kwa madai kuwa Wizara ya Fedha haijatoa fedha, kama ambavyo Bunge la Uganda lilivyoagiza kwenye bajeti.
“Kama kwa vijana wa U23, hatuna chaguo jingine ila kuwaondoa Uganda Cranes kwenye fainali za CHAN kwa sababu Wizara ya Fedha haijatoa fedha kama ilivyoidhinishwa na Bunge,” ilieleza taarifa yake na kuongeza:
“Vikwazo kwa Uganda vitaathiri siku zijazo, ikiwa hatutachukua uamuzi mgumu sasa pole kwa wachezaji na makocha waliofuzu timu lakini ni wakati wa kukabiliana na ukweli.”
Uganda Cranes imefuzu kwa fainali za CHAN 2022, nchini Algeria baada ya kuishinda Tanzania kwa jumla ya mabao 4-0.
Michuano ya CHAN 2023 inatarajiwa kuanza Januari 13 nchini Algeria. Uganda Cranes wako Kundi B pamoja na DR Congo, Ivory Coast, na Senegal.