Uhaba wa vyoo unavyochangia matatizo ya figo kwa watoto
REHEMA Emanuel alikuwa ni binti mwenye afya njema akisoma katika shule ya msingi Gidbiyo iliyo kilomita sita kutoka Babati Mjini mkoani Manyara, kaskazini mwa Tanzania. Alikuwa akicheza mpira wa pete, akiwa na marafiki wengi na alitarajia kuhitimu elimu yake ya msingi mwezi Oktoba.
Wakati wa majira ya kiangazi mwaka 2018 alipatwa na homa kali iliyolazimu alazwe, lakini kutokana na umri wake hakuna aliyedhani Rehema anaweza kuwa na tatizo kubwa. Alipewa dawa za kutuliza maumivu na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Hali hiyo iliendelea kujirudia na baada ya kubadili hospitali, Rehema ambaye ni mtoto wa pili kati ya watoto 10 wa mzee Emanuel alibainika kuwa na maambukizi katika njia ya mkojo (UTI). UTI kitaalamu ni maambukizi ya kawaida ambayo hutokea wakati bakteria, mara nyingi kutoka kwenye ngozi au rektamu, kuingia kwenye urethra, na kuambukiza njia ya mkojo.
Wataalamu wa Afya wanakiri kuwa watoto ni moja ya makundi yanayo athirika zaidi na UTI na kuwasababishia matatizo ya figo. “Hatukupata maelezo yoyote kutoka hospitalini,” anakumbuka mama yake. Siku moja anasema, “tulirudishwa nyumbani lakini hali ya Rehema haikuwa vizuri.”
Baba wa Rehema ni mkulima anayetegemea kuendesha familia yake na maisha yake kupita kilimo. Hana kazi mbadala ya kumuingizia kipato. Katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo ya kushuhudia mtoto wake akitaabishwa na homa aliona tatizo jingine.
Rehema alikuwa ameanza kupata na tatizo la ajabu, hakujua nini. Anasema alikuwa akiamka asubuhi miguu ikiwa imevimba na ikifika mchana hali inareja kawaida.
“Mimi sikuona tatizo lolote,” hata hivyo tumbo lilikuwa likiuma kila mara,” anasema Rehema. Tatizo la kuvimba lilendelea na mwaka 2019, Rehema anakumbuka kuwa aliamka mwili mzima ukiwa umevimba, ndipo alipopelekwa hospitali na kubainika na tatizo la figo.
Dada yake Rehema, Neema anakumbuka kuwa mdogo wake alikuwa mwenye kufadhaika, alikuwa amelegea na muonekano wake ulikuwa umeanza kubadilika. Hivi vikiwa ni viashiria vya shinikizo la damu.
Daktari Bingwa wa Watoto na Figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Jacquline Shoo, anasema uchafu katika vyoo hurahisisha maambukizi ya njia ya mkojo hasa kwa watoto na zaidi wale wa jinsia ya kike.
Dk. Shoo anaeleza kuwa, kwa kawaida kuna watoto wenye kinyaa. “Wao hubana mkojo ama akienda msalani hukuta kuna foleni na hivyo kushindwa kukojoa kwa wakati.” Mkojo unapokaa muda mrefu hugeuka sehemu ya kuitisha wadudu. Na kiafya, Dk Shoo anasema, mtoto anapaswa kukojoa kila baada ya saa mbili vinginevyo wale wadudu wanaota.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET) inaonyesha kuwa asilimia 32 ya shule Tanzania hazina maji safi, wanafunzi wanaolazimika kutumia maji kutoka vyanzo visivyo salama.
Pia asilimia 13 za shule hazina vyoo na asilimia 33 hazina vifaa maalum vya maji tiririka kwa ajili ya kunawa mikono kitendo ambacho kinachangia magonjwa ya kuambukiza yanayopelekea mdondoko wa elimu.
Aidha, Kwa mujibu wa kitabu cha Takwimu za Msingi nchini Tanzania cha Mwaka 2021 kilichotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa – NBS, mwaka huu, Idadi ya Shule za Msingi nchini Tanzania ilifikia 18,554 mwaka 2021 kutoka shule 18,152 mwaka 2020. Ongezeko hili pia liliendanda na ongezeko la idadi ya watoto waliosajiliwa katika shule hizo ambapo walifikia wanafunzi 10,687,593. Hili ni ongezeko la asilimia 2.1 kutoka wanafunzi 10,460,785 walioandikishwa mwaka 2020.
Hata hivyo ongezeko wa idadi ya shule na wanafunzi halijaendana na kasi ya kujenga idadi ya matundu ya vyoo. Taarifa za Elimu Msingi (2020) zinaonesha kuna upungufu wa matundu ya vyoo 181,000 sawa na asilimia 62.
Hii inafanya uwiano wa wanafunzi kwa tundu la choo kuwa 1:62 badala ya 1:25 kwa wavulana na 1:59 badala ya 1:20 kwa wasichana.
Rehema alikuwa miongoni wa watoto wa kike wanaopitia mazingira magumu wakiwa shuleni kutokana na idadi kubwa ya vyoo kuwa vichafu. Wataalamu wa afya, wanasisitiza wakati wote vyoo vinapaswa kuwa safi kwa kutumia maji tiririka na si maji ya kopo.
Mtaalamu wa Afya ya Mazingira Sarah Pima, anaeleza kuwa, mtoto mwenye maambukizi anapotumia kopo na kisha kushika mlango huacha vijidudu katika mlango. Vilevile, mtoto mwingine akiingia na kushika ule mlango hubeba vile vijidudu.
“Wakati mwingine watoto wala hawanawi vizuri mikono kwa maji tiririka hivyo bila kujua atamshika mwenzake na mwenzake,” amesema na kuongeza kuwa “watoto wengi wameathirika kwa maana ya kuwa na maambukizi kwenye njia ya mkojo bila kujua na wakati mwingine kuwa na presha.” Hao watoto hawajulikani kwa sababu hawaoneshi dalili yoyote.
Mtaalamu huyu anakubaliana na mawazo ya Dk Shoo kuwa uchafu wa vyoo huwafanya watoto wengi kubana haja hali ambayo ni hatari kwa afya zao.
“Usafi lazima uwe kitu cha kwanza. Kwa kuwa bakteria yupo kwenye kinyesi, kinapokaa pale kwa muda mrefu hasa akiwa ni mtoto wa kike, kinapata nafasi ya kupanda na kurudi kwenye njia ya mkojo kwa sababu zile njia zimekaa karibu, hivyo ni rahisi kwa yeye kupata UTI,” anasema.
Maambukizi ya magonjwa kama UTI yanayojirudia na kuharisha kunakotokana na homa ya virusi kunaweza kusababisha magonjwa ya figo.
“Tatizo la figo kwa watoto ni kubwa,” anasema Dk Shoo. Takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili zinaonesha kuna kliniki ya watoto wenye matatizo hayo kila Jumanne na Alhamis, ambapo asilimia 10 au watoto 30 wana magonjwa ya kudumu ya figo.
Tatizo hili pia linaweza kuwakumba vichanga na watoto wadogo chini ya miaka mitano. Wataalamu wanatahadharisha kuwa, kumuacha mtoto na chupi au nepi aliyoikojolea kwa muda mrefu humuweka mtoto katika hatari ya kuambukizwa UTI.
Vilevile, kumsafisha mtoto haja kubwa kwa njia ambazo sio sahihi husababisha mtoto kupata maambukizi.
Mwanafunzi wa Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Mkako, Japhet Mahinya, anasema uhaba na uchafu wa vyoo unawafanya baadhi ya wanafunzi kujisaidia juu ya uchafu hali inayochangia kuwafanya waugue matumbo mara kwa mara.
Katika Shule ya Msingi Halale, mwanafunzi Bonita Mwingira, anasema: “Mazingira ya vyoo ni machafu, tunakutana na kinyesi tunapoenda kujisaidia.” Hali ni mbaya zaidi kwa watoto wa awali wanaochangia vyoo na wanafunzi wa madarasa ya juu.
Katika shule hii, HabariLEo imeshuhudia matundu ya vyoo hayakidhi idadi ya wanafunzi na vifaa vilivyopo vya usafi ni vichache. Mwanafunzi mwingine, Pendo Michael, wa darasa la pili shuleni hapo anasema, mazingira ya vyoo ni machafu, hakuna maji na wanalazimika kujisaidia sehemu chafu yenye harufu kali.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Halale, Gaudence Luambano, anasema shule ina wanafunzi ni 722 wa kiume wakiwa 374 na wa kike 362. Anasema wanakabiliwa na changamoto ya uchache wa matundu ya vyoo kwani yaliyopo ni 14 huku kukiwa na upungufu wa matundu 18.
Sauti ya Afisa Elimu Kata, Mwl. France Komba
“Matundu yaliyopo pia yanatumiwa na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao ni 130 na wanafunzi wengine wakubwa,” anasema. Matumaini ya Mkuu huyu wa Shule ni kuwa wazazi waendelee kuwapima watoto wao na kuwatimu wakati serikali ikipanga kuboresha mazingira ya shule. Hii ni pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo.
Lakini wazazi wanafikra tofauti. Wanaamini ni wajibu wa serikali kuhakikisha mazingira ya shule ni salama kwa walimu na watoto. “Jukumu la mzazi ni kusaidia mahitaji madogo ya mwanafunzi,” anaeleza mmoja wa wazazi, Adeliheri Newa.
“Tofauti na sehemu zingine, watoto hapa wanasumbuliwa na maradhi ya homa ya tumbo mara kwa mara na ukienda hospitali lazima utakuta UTI.” Hali ni mbaya zaidi kama hakuna maji, wanafunzi na walimu katika shule hii wanasema.
“Kila siku UTI. Tunaomba serikali isaidie kuweka mkakati utakaowezesha upatikanaji wa maji muda wote na ufanyike ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha vyoo ni visafi,” alishauri Newa. Mkazi wa Lipokela, Rhaiman Salum, anasema anatamani elimu ya afya itolewe zaidi kwa walimu ili watambue madhara ya UTI Sugu kwa watoto na kupambana na tatizo hilo.
NDOTO ZA ZIMA
Ndoto za Rehema kuendelea na shule zimezima. Haijui kesho yake na sasa amekuwa ni yeye na hospitali, hospitali na yeye. Makazi yake mapya ni Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa Dodoma.
Neema, Dada yake anasema yeye pia ameshindwa kuendelea na masomo ili amhudumie mdogo wake. Neema na Rehema wamepanga nyumba mjini Dodoma ili waweze kuhudhuria kliniki ya figo ambayo inahusisha kusafisha damu ‘dialysis’ mara tatu kwa wiki. Gharama za huduma hii ni Sh 250,000 kwa kila awamu ambayo ni sawa na Sh 750,000 kwa awamu tatu kwa wiki.
Matumaini ya Rehema ilikuwa siku moja awe Mwalimu, lakini hana matumaini tena. Wakati serikali inahimiza watoto wa kike kwenda shule, Rehema anawaza ataamkaje Kesho.
Familia ya Rehema imeipongeza serikali kwa kutoa msamaha wa matibabu. Kwa sasa Rehema analazimika kulipia Sh250,000 kwa wiki huku Sh500,000 zikilipwa na Serikali. Hata hivyo familia hii inaona bado mzigo ni mkubwa, ukizingatia baba ni mkulima na ana watoto wengine tisa wanaomtegemea.
Mariam Said, mkazi wa Mwananyamala anayeuguza mtoto wake mwenye tatizo la figo katika kitengo cha Figo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anasema kuna changamoto nyingi kulea mtoto mwenye tatizo hilo likiwamo suala la kutumia muda mwingi na pesa nyingi, badala ya kufanyakazi nyingine za kijamii na kiuchumi.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Onesmo Kisanga kwa upande wake anasema “UTI’ ni moja ya chanzo cha uharibifu wa figo kwa kuwa protini inapopita kwenye mkojo inasababisha presha kupanda, na presha ikiwa juu hupelekea figo kushindwa kufanya kazi.
Kwa takwimu za Wizara ya Afya za 2021 zimebainisha kuwa takriban Watanzania 5800 mpaka 8500 wakubwa kwa wadogo wanahitaji huduma ya kusafisha damu yaani dialysis au huduma za kupandikizwa figo.
WANAFUNZI WENGI WAPO HATARINI
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Juhudi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Devotha Mgaya, anasema hali ya upatikanaji na utumiaji wa vyoo hairidhishi kwa kuwa vyoo vilivyopo havina maji tiririka. Wanafunzi hapa wanatumia ndoo zinazojazwa maji yanayochotwa mtoni.
Kwa mujibu wa Ofisa Elimu wa eneo hili, France Komba, shule hiyo ina wanafunzi 875 wanaohitaji matundu 33 ya vyoo, lakini yaliyopo ni 18 yanayotumiwa na wanafunzi wakubwa na wadogo.
Aidha, Mwalimu wa Afya na Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkako, Jamila Ngole, anasema maambukizi ya UTI yapo na mara kwa mara watoto wanalalamika kuugua matumbo. “Wanapoenda kupimwa, mrejesho tunaopata kutoka kwa wazazi ni wengi kugundulika kuwa na UTI,” anasema Ngole.
Mwalimu Ngole anasema wameweka mkakati wa kufanya usafi kwa kushirikiana na wanafunzi mara tatu kwa siku kwa kutumia maji safi na sabuni ya unga au maji na majivu. “Tumewaelekeza watoto kuhakikisha wanamwaga maji kabla na baada ya kujisaidia,” alisema.
SERIKALI YAANZA KUCHUKUA HATUA
Serikali inasema imeanza kuboresha shule za Tanzania kupitia mradi wa Boost na imetenga bajeti ya Shilingi Trilioni 1.15 katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Vile vile, aliyekuwa Waziri Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa alibainisha kuwa kupitia bajeti inayoandaliwa kwa mwaka 2022/23 wataweka kipaumbele cha kukabili upungufu wa matundu ya vyoo hasa kwa shule za msingi itakayokwenda sambamba na kupunguza uhaba wa nyumba za walimu.
Katibu Mkuu Tamisemi, anayeshughulikia Elimu, Charles Msonde akizungumza na Habarileo anasema serikali inatambua upungufu uliopo wa miundombinu ya choo na uchakavu wa majengo ya madarasa kwa baadhi ya shule.
“Serikali tayari tumefanya tathmini Kwa shule zate zote za Awali na Msingi, kuna shule ambazo zinaidadi kubwa ya wanafunzi kuzidi 1500 kwenye darasa moja, kwa mwaka huu imetengwa shilingi bilioni 230 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya madarasa na matundu ya vyoo.”Amesema
USHAURI WA WADAU
Mwenyekiti wa Bodi ya HakiElimu, Richard Mabala amesema serikali haina budi kuweka kipaumbele cha afua za afya mashuleni, sio tu itasaidia mwanafunzi kiafya pia kiakili. “Kuna baadhi ya shule hazina vyoo wanajisaidia vichakati, nyingine vyoo havitoshi, wapo wanaolazimika kujibana, Ile ni ‘call of nature ‘ kuzuia kinachotakiwa kutoka ni hatari kiafya na maumivu yake ni makubwa.” Amesema Mabala