Uhakiki uanachama wa Somalia EAC waanza

Uhakiki uanachama wa Somalia EAC waanza

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), imeanza mchakato wa uhakiki kwa Shirikisho la Somalia kuwa mwanachama mpya wa jumuiya hiyo, baada ya Taifa hilo kutuma maombi ya kujiunga hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Dk Peter Mathuki, amesema mchakato wa Somalia kujiunga na jumuiya hiyo umeanza leo baada ya timu maalum kutoka sekretarieti ya EAC kwenda Somalia kukaa pamoja na wataalamu wa serikali ya nchi hiyo, ili kuona utayari wa kujiunga na EAC.

“Baada ya kukutana pamoja wataandaa ripoti na kuipeleka Baraza la Mawaziri wa EAC wanaotarajia kukutana Februari 23 mwaka huu na kisha kupelekwa ripoti hiyo kwenye mkutano wa wakuu wa nchi utakaofanyika Februari 25 kwa ajili ya hatua zinazofuata,” amesema.

Advertisement

“Mchakato wa nchi hiyo ulishaanza siku za nyuma na jana sekretarieti imetuma timu ya wataamu wa EAC na wameenda kuonana na wataalamu wa serikali ya Somalia kuona utayari wao kuomba kujiunga na EAC, kisha hatua zingine zitafuata kwa jinsi wakuu wa nchi watakavyoona,'”alisema.

Mathuki amewatoa hofu wanajumuiya ya EAC kutokuwa na woga kwa nchi ya Somalia kujiunga na EAC, kwani kuna fursa za kiuchumi nyingi zitaongezeka na vijana wa nchi wanachama watapata ajira kutokana na jumuiya hiyo kukua.

Amesema kuhusu changamoto za kiusalama zilizopo kwa baadhi ya nchi hizo, wanamaini watakapojiunga ndani ya EAC itakua rahisi kuzishughulikia na kuhakikisha wananchi wanakuwa katika hali ya amani.