Uhamiaji wakabidhiwa gari kudhibiti wahamiaji haramu

KAGERA: Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amewakabidhi gari ldara ya Uhamiaji Mkoa wa Kagera ili kuendelea kudhibiti wahamiaji haramu mkoani wa Kagera.
Akikabidhi gari hilo leo aina ya ‘Fortuner’ RC Mwassa amesema kutokana na tatizo kubwa la wahamiaji haramu mkoani humo na Idara ya Uhamiaji kuwa na vitendea kazi vichache wameona haja ya kumwomba Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA asaidie upatikaji wa vitendea kazi hususani magari.
“Hili gari ninalolikabidhi leo Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kagera tumelipata kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania baada ya kumuomba atusaidie kutatua kero ya wahamiaji haramu katika mkoa wetu ambapo alinikubalia na kutupatia magari mawili moja likiwa tayari tumelipokea na leo tumepokea hili,”alisema Mwassa.
Ametoa wito kwa watanzania kuacha utamaduni wa kiwakaribisha wanachi wa nchi nyingine kienyeji kwani baadhi huja kwa ajili ya kufanya vibarua na badae ulowea na kuanzisha familia zao na hali hiyo uchangia ongezeko kubwa la wahamiaji na kuwahamisha inakuwa ngumu.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kagera Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Iraneneus Kasimbazi akieleza juu ya tatizo la Wahamiaji haramu alisema kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Agosti 2025 Idara imewakamata wahamiaji haramu 10,960 na waliorudishwa katika nchi zao mpaka sasa ni zaidi ya 9,000
Amesema kuwa waliofikishwa mahakamani ni 500 huku akidai kuwa kuwatunza ni gharama zaidi kwani wimbi la wanaongia ni kubwa na wakiingia mara nyingi gharama za kuwarudisha ni kubwa ,kuwatunza wakati wa kesi , kuwapa chakula pamoja na kutafuta wakarimani wa kutafsiri lugha ili kuwaelewa
Amesema ombi la sasa ni kuomba basi la kuwasafirisha kuwarudisha kwenye nchi zao pale wanapokamatwa ambapo amedai kuwa Upatikanaji wa gari Hilo ni msaada mkubwa sana kwao na litaongeza utendaji kazi katika idara Hiyo.
Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Castro John kwa niaba ya kamishina mkuu alisema kuwa mapato ya Serikali hayawezi kukusanywa mkoa usipokuwa na utulivu wa kutosha na upatikanaji wa gari hilo utaimarisha utulivu wa mkoa.
Amesema atawasilisha maombi ya idara wa Uhamiaji yanayohusu Vifaa ili idara hizo ziendelee kushirikiana kwani uwepo wa wahamiaji wengi unaathiri shughuli za ukusanyaji mapato na kudai kuwa kama idara hiyo itakuwa na vitendea kazi imara na Swala la wahamiaji likadhibitiwa basi mapatao yatakusanywa zaidi .



