WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma, iko katika hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa barabara ya mchepuko maarufu Mtwara corridor yenye urefu wa kilometa 14.3.
Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Ruvuma, Ephatar Mlavi alisema barabara hiyo ni sehemu ya ujenzi wa mradi wa barabara kuu ya Songea-Makambako.
Kwa mujibu wa Mlavi, ujenzi wa barabara hiyo utaanzia eneo la Namanditi ambapo itapita kata ya Mwenge msindo, Msamala, kituo cha kupoza umeme Unangwa hadi Changarawe, barabara kuu ya Songea-Tunduru.
Alisema barabara hiyo itakapojengwa, itasaidia kuondoa msongamano wa magari katikati ya mji wa Songea hasa malori yanayobeba makaa ya mawe.
“Barabara hii ya mchepuko ina umuhimu mkubwa na itaongeza fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na wale wanaofika kutoka mikoa mingine,” alisema Mlavi.
Alisema tathmini ya fidia kwa ajili ya kuwalipa wananchi watakaopitiwa na mradi huo imeshafanyika na sasa serikali iko katika hatua ya mwisho ya malipo ili wananchi waweze kupisha ujenzi wa mradi huo.
Barabara hiyo itapita katika vijiji vitano vya Namanditi, Luwawasi, Mtaungana, Osterbay na Kuchile.
Baadhi ya wananchi waliomba serikali kuanza ujenzi haraka iweze kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na kuharakisha maendeleo yao.