Ujenzi bonde la Msimbazi wanukia

ILI serikali itekeleze Mradi wa Bonde la Msimbazi Dar es Salaam, ni lazima kuwahamisha watu wanaoishi maeneo hatarishi na baadhi wenye makazi maeneo salama. Lengo la kuanzishwa mradi huo ni kukabiliana na mafuriko katika bonde hilo na kuboresha matumizi ya ardhi katika eneo la chini la bonde.

Serikali ilianza rasmi kazi ya uthamini kwa kushirikiana na Norplan, Novemba mwaka juzi kwa wakazi wa maeneo yanayoathiriwa na mafuriko. Mratibu Msaidizi wa mradi huo, Nyariri Kimacha, anasema hatua iliyofikiwa kwa sasa katika mwezi huu wa Oktoba ni wananchi waliopo katika eneo hilo la mradi kuanza kulipwa fedha zao za fidia. “Serikali imeshakabidhi fedha za kulipa fidia.

Ndani ya mwezi huu wa 10 fedha hizo zitaanza kulipwa,” anasema Kimacha. Mtaalamu wa Masuala ya Kijamii kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Beatrice Mchome anasema wamempata na kumtambulisha rasmi mshauri wa kutekeleza uratibu huo kwa wananchi wanaosubiri fidia.

Anawaeleza wananchi tayari tangazo limeandaliwa kutaarifu kuwa sasa zoezi la kupokea fidia limefika, watajulishwa tarehe na wapi. Pamoja na utaratibu huo ulioandaliwa anaeleza Tamisemi itakusanya taarifa ya watoto wa shule ili isilete usumbufu katika masomo yao.

“Tutakusanya taarifa ili zisaidie mambo mbalimbali ikiwemo taarifa za watoto wa shule ili Tamisemi ione namna watoto hawa watakavyohamishwa shule bila usumbufu,” anasema. Kwa maelezo yake, mpango wa ardhi mbadala umefanyika kwa wananchi watakaopenda kwenda katika maeneo hayo ikiwemo Mvuti, Kigamboni na Tegeta ambako wananchi walipelekwa kuona.

“Kwa mara ya kwanza mradi mkubwa unatekelezeka mara moja zaidi ya watu 3,000 wanahama katika bonde hilo,” anasema Mchome. Kwenye jambo lolote la kimaendeleo hapakosi malalamiko kutoka kwa wananchi kama ilivyotokea katika eneo hilo pale makosa ya kibinadamu yalipotokea na kutolea mfano labda mtu alisahaulika kuwekewa posho ya pango.

“Tuliona tukirekebisha suala moja linazua mengi tukasitisha zoezi ila hatukusitisha kupokea malalamiko ya wananchi. Na serikali haiwezi kutekeleza mradi bila kufuata sheria ya nchi,” anasema. Naye Mshauri wa masuala hayo ya fidia kutoka Kampuni ya Property Matrix Co. Limited (PML), Charles Mhando anaeleza anatarajia kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wakubwa wa mradi ambao ni wabunge, madiwani na wenyeviti wa mitaa.

Ushirikiano mwingine anautegemea kutoka kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ofisi za wakuu wa wilaya, za wakurugenzi wa halmashauri, watumishi wa serikali, watendaji wa kata na mitaa, Tamisemi na wananchi wanaoguswa na mradi. Kwa maelezo yake mpaka sasa uthamini ulishafanyika kwa watu 3,552 na kuandaliwa kwa taarifa ya uthamini wa majedwali ya fidia.

Naye Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba anasema hakuna anayekataa kazi ya uboreshaji wa bonde hilo kwa kuwa utaboresha maisha ya watu, miundombinu na kuondoka katika hatari wale waliokuwa wakiishi maeneo yenye mafuriko kila wakati.

Gharama za mradi ni takribani Dola za Marekani milioni 260 ambapo Benki ya Dunia inatoa mkopo wa Dola milioni 200, Serikali ya Hispania inatoa mkopo wa Dola milioni 30 na Serikali ya Uholanzi inatoa ruzuku ya Euro milioni 30.

Mradi utatekelezwa kwa muda wa miaka sita kuanzia mwaka huu na una sehemu kuu nne ikiwemo miundombinu kwani katika eneo hilo litaboresha miundombinu kwa ajili ya kukabiliana na mafuriko ikiwemo kupanua na kuongeza kina cha Mto Msimbazi, kupanua mawanda ya mafuriko, kujenga maeneo salama kwa makazi na biashara (hekta 57) na bustani ya Jiji.

Pia mradi utajenga daraja jipya la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na kujenga karakana mpya ya mabasi yaendayo haraka katika eneo la Ubungo Maziwa. Kwa juu ya bonde, Mchome anasema mradi unatarajia kuboresha misitu ya Pugu na Kazimzumbu, kuimarisha kingo za Mto Msimbazi katika maeneo korofi, kuanzisha programu za usimamizi wa taka ngumu katika makazi yaliyopo karibu na bonde.

Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wanatarajia kuanza ujenzi Januari 2024. Kwa sasa taratibu za manunuzi ya kuwapata mtaalamu mshauri na mkandarasi wa kujenga daraja jipya la Jangwani tayari zimeshaanza. Kuhusu fidia, Mchome anasema kaya 2,592 zimetambuliwa kuwa katika eneo linalokumbwa na mafuriko na kaya 314 zimetambuliwa kuwa zitaathirika na ujenzi wa maeneo salama ya makazi na biashara.

Anasema uthamini wa mali za waathirika ulifanyika Novemba 2021 kwa kaya zilizo kwenye mafuriko na Desemba 2022 kwa kaya zinazoathirika na ujenzi. Anaeleza mnamo Machi 2023, kaya zilizo kwenye mafuriko zilihakiki fidia zao baada ya uthamini ambapo kaya 2,214 zilikubaliana na kiwango cha fidia kilichothaminiwa na kaya 167 hazikukubaliana na kiwango cha fidia. “Kaya 211 hazikufika katika zoezi la uhakiki wa viwango vya fidia,” anasema

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x