Ujenzi Bwawa la Yongoma mbioni

SERIKALI kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 imepanga kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na ujenzi wa Bwawa la Yongoma lililopo wilayani Same kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kuinua kipato cha wakulima.

Hayo yamesema na Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde alipofanya ziara ya kikazi wilayani Same kukagua maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji na miundombinu yake katika kata  za Ndungu,Miamba na Kihurio.

Mavunde amesema “Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaendelea kukipa kilimo kipaumbele cha juu, ambapo bajeti ya mwaka 2023/2024 ametutengea fedha kiasi cha bilioni 970, kati ya fedha hizo zaidi ya sh bilioni 384 zimeelekezwa kwenye umwagiliaji”

Advertisement

Amesema, msukumo mkubwa kwenye kilimo unaooneshwa na Rais Samia ndio  unapelekea Tume  ya Taifa ya Umwagiliaji kuendelea na ujenzi wa skimu, visima na mabwawa nchi nzima ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao nchini.

“Tumesikia kilio cha wakulima wa Ndungu juu ya ukarabati wa skimu hii,katika bajeti ya mwaka 2023/24 tumetenga fedha za ukarabati na ujenzi wa Bwawa la Yongoma.” Amesema

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Anne Kilango-Malecela wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyoendelea kuwakumbuka wananchi wa Same kupitia miradi hiyo  ya umwagiliaji.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa alibainisha kuwa pamoja na upembuzi yakinifu, usanifu na ujenzi wa bwawa la Yongoma, Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2023/24 pia itafanya ukarabati wa mifereji ya skimu ya Ndungu ambayo inatoa maji mto Yongoma ili kuhakikisha wakulima 3000 wanufaika na uzalishaji wenye tija kwenye hekta 680 za skimu hiyo.

Amesema, serikali pia  itaendelea na ujenzi wa mifereji ya maji katika eneo la miamba na kusanifu bonde la mto saseni ili wananchi zaidi ya 68,000 wanufaike na kilimo cha umwagiliaji.

3 comments

Comments are closed.