Ujenzi ofisi ya Machinga Geita yafikia asilimia 40

HALMASHAURI ya Mji wa Geita imeweka wazi kuwa utekelezaji wa agizo la Rais wa Tanzania, Samia Suluhu juu ya ujenzi wa ofisi za Shirikisho la Umoja wa Machinga Mikoa (SHIUMA) umefikia asilimia 40.

Ofisa biashara Halmashauri ya Mji wa Geita, Said Mwalanga amebainisha hayo leo katika taarifa yake kwa mkuu wa mkoa wa Geita alipofika kukagua mradi huo.

Amesema ofisi za shiuma mkoa wa Geita zinatarajiwa kugharimu jumla ya Sh milioni 38.7 kwa kujumuisha ujenzi wa jengo la vyumba vitatu, ukumbi, choo cha matundu matatu na kitako cha tenki la maji.

Advertisement

Amesema bajeti hiyo inazingatia mchoro na makadirio ya vifaa kutoka wizarani na ofisi itajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inazingatia bajeti ya Sh milioni 10 iliyotolewa na ofisi ya Rais kwa kila mkoa.

“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa ofisi ya Shiuma imeanza rasmi Juni 9, 2023 na itakamilika Juni 29, 2023. Halmashauri imetenga fedha mwaka ujao wa fedha kukamilisha awamu ya pili ya ujenzi wa ofisi hiyo.”

Mkurugezi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahra Michuzi amesema wamejipanga kukamilisha mradi huo kwa ufanisi ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu kuwatengenezea mazingira rafiki ya biashara machinga.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Barnabas Mapande amepongeza Rais Samia kwani hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM kuwasaidia wajasiliamali wadogo kufanya kazi zao kwa tija na katika mfumo rasmi.

Mwenyekiti wa Shiuma mkoa wa Geita, Masoud Ally ameishukuru serikali na kueleza ujenzi wa ofisi za machinga utaondoa changamoto ya Shiuma kukosa eneo maalum la viongozi na sasa watafanya kazi kwa mfumo rasmi

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela ameelekeza mradi ukamilike kwa wakati ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo kupata sehemu maalum ya kuwasilisha kero zao kabla ya kupelekwa kwa viongozi wa ngazi za juu.

/* */