KIPANDE cha ujenzi wa reli ya kati Tabora- Kigoma kitagharimu dola za Marekani bilioni 2.7 sawa na shilingi trilioni 6.34.
Reli hiyo ambayo mkataba wake umesainiwa leo Desemba 30, 2022 SGR LOT 6 (Tabora – Kigoma) katika Ukumbi wa Kikwete – Ikulu jijini Dar es Salaam, itachukua miezi 48 kukamilika.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba kusaini kipande hicho, serikali itakuwa imewekeza dola za Marekani bilioni 10.04, sawa na Tsh, Trilioni 23.3 kwa maana ya awamu ya Dar-Mwanza na Tabora-Kigoma.
Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa amesema utiaji saini huo wa leo unafanya utimilifu wa reli ya kati, kutoka Dar- Mwanza na Dar-Kigoma, kwingine kote kutakapofuata ni reli za matawi.
“Mheshimiwa Rais ulisema tuanze kujenga reli kuelekea DRC kwa kuwa tusipofanya hivyo wenzetu watajenga, kwa ujenzi huu wa jumla wa kilometa 2,102 unaifanya Tanzania kuwa nchi yenye ujenzi wa SGR ndefu kuliko zote Afrika,” amesema Kadogosa na kuongeza:
“Reli ya SGR itaunganisha bandari ya Dar, DRC kupitia bandari ya Kigoma, hivyo katika miji mikubwa ndani ya DRC tutakuwa tumefikia kufikia miji ya Uvila, Bukavu, Kalemie, Lubumbashi na Goma, tutakua tumefikia miji mitatu yenye ‘population’ kubwa ya watu, hiyo ni fursa kwa wafanyabiashara,” amesema.
Amesema Ujenzi wa Tabora-Kigoma una kilometa 506, utakuwa na stasheni 10, vituo vikubwa vya mizigo Uvinza na Katosho.
Kadogosa amesema mikataba yote iliyosainiwa haitakuwa na mabadiliko ya bei, mfano bei ya vitu vya ujenzi ikibadilika na bei ibadilike, hiyo haitakuwepo.
“Kama tungekubali hilo inamaanisha kuwa kungekuwa na nyongeza ya zaidi ya dola bilioni 1.304. Hii ina maana kungekuwa na ongezeko la asilimia 30.3 kwa maana ya thamani ya fedha,” amesema.
Amesema serikali inaendelea na ununuzi wa vitendea kazi, na kwamba tayari wamenunua mabehewa 59, ambapo tayari mabehewa 14 mapya yameingia, kuna mabehewa 30 na vichwa viwili ‘used’ vitaingia kati ya Machi au Aprili 2023.
“Tulikuwa na matatizo na msambazaji wa kwanza wa Uturuki, tuliamua kuvunja mkataba baada ya kushauriana serikalini, tukampa mtu mwingine aliye Ujerumani kwa ajili ya kumalizia kazi, tulifanya maamuzi hayo kwa nia njema,”amesema.
Amesema vichwa vya treni 17 kutoka Korea Kusini, vitaanza kuingia Juni 2023, kuna seti 10 ya treni za kisasa (EMU), ambapo seti mbili za kwanza zinaingia Juni 2023.
“Tuna mabehewa ya mizigo 1430 kutoka China, yataingia nchini Septemba 2023, kuna vifaa kutoka Korea Kusini, hivyo uwekezaji huu kwa jumla unafanya kuwa na thamani ya jumla Dola milioni 557.731 sawa na shiingi Trilioni 1.29.
“Niweke wazi pia tenda ya ununuzi ilitangazwa mara mbili lakini hatukupata mtu wa uhakika, tukaamua kwenda kwa mzalishaji moja kwa moja,” amesema.
Amesema kuna kampuni kutoka Urusi, Korea Kusini, Japan, Ujerumani, Uholanzi, Malaysia ambazo zilifuata taratibu zote na mwisho wakapata ‘lowest evaluated bidder’ lakini kwa kujali ubora na kujali mahitaji waliyowaambia.
“Hivyo, yanayozungumzwa kuhusu bei ni mambo ya mitandaoni tu,” amesema Kadogosa
Wakati huo huo Kadogosa amesema mbali na ujenzi wa miundombinu, TRC kwa kushirikiana na TANESCO wanajenga laini ya umeme wa kujitegemea, kwa maana kutakuwa na laini ya TRC yenyewe haitaingiliana na laini yoyote kwa ajili ya kupata umeme wa uhakika.
“Tunafurahi kwa kuwa ndani ya siku mbili hizi tutakuwa na mchakato wa kujaza maji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, na sisi tutaenda,” amesema