Ujenzi sekondari Kigera bado kidogo tu!

UJENZI wa sekondari mpya ya Kata ya Kigera, Manispaa ya Musoma, mkoani Mara  inayotakiwa kuanza usaili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari mwakani, umefikia hatua nzuri.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bosco Ndunguru katika mahojiano maalumu na HabariLEO, Ofisa Uchumi wa manispaa hiyo, Joseph Ochora amethibitisha kuwa usaili wa wanafunzi hao utafanyika kama ilivyokusudiwa.

Amesema mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Mpango wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQIP), ulitengewa jumla ya Sh Milioni 600, ambapo Februali mwaka huu walipokea Sh.Milioni 470.

Hata hivyo kwa sasa ujenzi hauendelei kutokana na Sh. Milioni 30.942 kufungiwa kwenye mfumo, mwisho wa Mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Ochora, taratibu za kutoa fedha hizo zimekamilishwa na ujenzi utaendelea wakati wowote kuanzia sasa.

Amesema bajeti ya mwaka huu wa fedha haijatenga fungu la ununuzi wa samani za shule hiyo, hivyo ili kufanikisha malengo manispaa imetenga Sh. Milioni 10 kutoka kwa mapato yake ya ndani, kwa ajili hiyo.

Hata hivyo amesema bajeti ya serikali ya mwaka huu wa fedha, imetenga Sh. Milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu wa shule hiyo.

“Yatajengwa majengo mawili yenye nyumba za kaya nne, yaani two in one mbili,” amesema Ochora.

Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Miundombinu na Maendeleo ya Mjini na Vijijini, Mhandisi Rafedi Jafet, akizungumza kwa niaba ya Nduguru ametaja majengo yaliyo kwenye hatua ya kumalizia kuwa ni madarasa nane, jengo la utawala, maktaba, maabara tatu za sayansi na matundu 27 ya vyoo.

“Fedha zilizokwama kwenye mifumo zikija, tutakamilisha ujenzi maana vifaa vyote vipo,” amesema.

Amesema msingi wa jengo la Tehama (ICT) umemwagwa jamvi, huku mfumo wa kuvuna maji ambao unatakiwa kuunganishwa na maeneo ya kunawia mikono, ukiwa haujaanza kujengwa.

Amesema kazi hizo zinatarajiwa kutekelezwa kwa kutumia Sh.

Milioni 130 ambazo hazijapokewa.

Habari Zifananazo

Back to top button