Ujenzi SGR  Mtwara-Mbamba Bay mwaka huu

WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi imesema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay-Songea-Ludewa mkoani Ruvuma unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024 kwa mfumo wa kushirikiana na sekta binafsi (PPP).

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayehusika na uchukuzi, Gabriel Migire alipozungumza na HabariLEO jana.

Migire alisema baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa mradi huo, hatua iliyopo sasa ni kumpata mtaalamu wa kuandaa nyaraka kwa ajili ya kupata wawekezaji wazuri kwenye mradi huo wenye urefu wa takribani kilometa 1,000.

Advertisement

Alisema nyaraka hizo zitatumika kupima utayari wa sekta binafsi ya ndani na nje kuwekeza kwa ubia na sekta ya umma (PPP) kwenye mradi huo, hivyo sekta binafsi watakapopata nyaraka hizo wajitokeze na kuomba.

“Utafiti uliofanyika ulionesha kwamba ni mradi ambao unaweza ukafanywa na sekta binafsi kwa sababu una faida, kwa hiyo nyaraka zitakazoandaliwa zitakuwa na lengo la kuuza mradi kwa sekta binafsi ambao wanaweza kuwekeza kwenye ujenzi kwa utaratibu tutakaokubaliana,”alisema Migire.

Alisema katika kufanikisha mradi huo watashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kwani kuna kitengo kinachohusika na ushirikishaji wa sekta binafsi kwenye masuala ya miradi ya ubia.

“Ni mradi ambao unalipa (una faida) kwa sababu kuna biashara, ukijenga unaweza ukaendesha ukajilipa badala ya serikali kwenda kuwekeza fedha peke yake, kwa kweli huu mradi upo kwenye vipaumbele vyetu kwa mwaka huu wa fedha tuliouanza,”alisema Migire

Kwa mujibu wa Migire, mradi huo ukitekelezwa utasaidia kuifungua Kanda ya Kusini kwa kusafirisha chuma, makaa ya mawe na mizigo itakayoingia kupitia Bandari ya Mtwara.

Alisema Bandari ya Mtwara pia ipo mahususi kwa ajili ya kuhudumia nchi za Malawi, kaskazini mwa Msumbiji na Zambia kwa kiasi fulani.

Kuhusu gharama za mradi huo, alisema hawezi kulisema kwa sasa mpaka hapo atakapopatikana mwekezaji ili asema atautekeleza kwa gharama gani japo serikali inajua kilometa moja inajengwa kwa kiasi gani cha fedha kutokana na uzoefu iliyonao wa kutekeleza miradi ya reli.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *