DAR ES SALAAM:Ujenzi wa Soko la Ndizi la Urafiki lililopo Halmashauri ya Ubungo mkoani Dar es Salaam umeanza rasmi, muda mchache baada ya uongozi uliokuwepo kuondolewa
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Hashim Komba amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo kuhusu ujenzi wa soko hilo ambalo awali lilimilikiwa na wafanyabiashara lakini sasa hivi limerudishwa serikalini.
Komba amesema sh milioni 600 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi katika Soko hilo ambao tayari umeanza na jengo la kwanza.
“Na kwa kuanzia imeshatengwa bajeti milioni 600 ambayo ndio inaanza kwa ajili ya kufanya maboresho na ukienda sasa hivi eneo lile ambalo wanauza ndizi utakuta tayari kuna jengo limeanza kujengwa la kwanza kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara waanze kukaa kwenye maeneo mazuri,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Amesema baada ya jengo hilo kukamilika ujenzi utaendelea kwenye majengo mengine pamoja na choo cha kisasa, ujenzi wa mitaro kwa ajili ya kuchepusha maji na eneo la maegesho ya magari.
Amesema ujenzi unaoendelea utasaidia kwa kuwa kipindi cha mvua wafanyabiashara wamekuwa wakifanya biashara kwenye matope, biashara zinakuwa juu ya matope na wateja wanaingia na kukanyaga matope.
“Tumekubaliana na wenzetu wa halmashauri kwamba tufanye maboresho, lengo ni kuhakikisha kwamba mazingira yale yanaboreshwa na wafanyabiashara wafanye biashara katika mazingira ambayo ni mazuri hicho ndicho ambacho kinaendelea kwa sasa.
“Tumejiwekea malengo katika kipindi cha miezi sita tuwe tumeshafanya maboresho. Hivi tunavyozungumza tayari jengo la kwanza linaendelea kwa hiyo likikamilika tunaingia jengo lingine,” amesema.
Amesisitiza kuwa kuelekea msimu wa mvua tahadhari zote muhimu zimechukuliwa za kuhakikisha ujenzi unakwenda kasi.
Amesema endapo soko lingekuwa wazi ujenzi ungeenda haraka zaidi lakini kwa kuwa wanajenga huku biashara zinafanyika lazima ukamilishe eneo moja unawahamisha wafanyabiashara kwenye eneo ambalo limekamilika huku ukibomoa eneo lingine kwa ajili ya kufanya maboresho.
“Tunataka biashara ziendelee na ujenzi nao uendelee ndio maana angalau tumejipa miezi sita tuende taratibu taratibu ili walau biashara za watu wetu ziendelee,” amesema.
Agosti 17 mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alivunja uongozi wa Soko la Mabibo na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufanya uchunguzi kwa kina katika soko hilo, watakaobainika kukiuka maadili ya uongozi wachukuliwe hatua.
Chalamila alivunja uongozi huo wakati akitatua mgogoro kati ya wafanyabiashara wasio waaminifu wakiongozwa na uongozi wa soko hilo na halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.