Ujenzi wa chuo kikuu Kagera kuanza Juni 1

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jakaya Kikwete 

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dare es Salaam (UDSM), ambaye Rais Mstaafu wa Awamu  ya Nne, Jakaya Kikwete, amesema ujenzi wa chuo hicho  tawi la mkoani Kagera utaanza Juni Mosi mwaka huu.

Kikwete alifanya kikao na viongozi wa Mkoa wa Kagera  na kuwahakikishia kuwa vikwazo ambavyo vingekwamisha ujenzi huo tayari vimetatuliwa, ambapo mpaka sasa hati za ujenzi zimekamilika na kilichabaki ni kuanza ujenzi wa tawi hilo la Dar es Salaam.

“Huwezi kujenga chuo kikuu au kupata fedha kama hauna hati za ujenzi, hati nne ambazo zilitakiwa zimekamilika na timu ya vijana wetu wanaopaswa kusanifu muonekano wa chuo kikuu wamefika na mimi nitaungana nao kwa ajili ya ukaguzi wa eneo, ” alisema Kikwete.

Advertisement

Alisema zaidi ya Sh Bilioni 18 zinatarajia kutumika ujenzi wa chuo hicho na matarajio yake makubwa na kuona baadaye chuo kinajitegemea  na kuwa chuo huru katika miaka ijayo.

Alitoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanatumia  chuo hicho kama fursa ya kujipatia elimu na kujiinua kiuchumi, huku akisisitiza serikali ya sasa inajaribu kutoa kipaumbele kwa masuala ya elimu.

Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, anayeshughulikia masuala ya taaluma, Boniventure Rutinwa, alisema mafunzo mbalimbali hasa ya uchumi elimu na mifumo yataanza hivi karibuni na masomo ya mwaka 2023/2024 yataanza kutolewa kwa  eneo la Bukoba, wakati ujenzi wa chuo unaendelea eneo la Chemba.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila alisema uwepo wa chuo hicho ni fursa kubwa kuhakikisha Mkoa wa Kagera unainua uchumi.