UJENZI wa Mradi wa Safari City tayari umeanza ambapo mamlaka zinazohusika zimeendelea na uwekaji wa miundombinu muhimu ya barabara, maji na umeme.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda wakati akijibu swali hilo la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Dk John Pallangyo (CCM) kwa niaba ya Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete.
Dk Pallangyo alitaka kujua ni lini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), litaanza ujenzi wa Safari City nje kidogo ya Jiji la Arusha.
“Ujenzi wa mradi wa Safari City tayari umeanza ambapo mamlaka zinazohusika zimeendelea na uwekaji wa miundombinu muhimu ya barabara, maji na umeme,” alisema.
Pinda alijibu kwamba mradi wa Safari City una jumla ya viwanja 1,713 kwa ajili ya uendelezaji wa nyumba za makazi, majengo ya biashara, maeneo ya viwanda vidogo vidogo na huduma za jamii kama shule, hospitali na maeneo ya kuabudia.
Pia mradi huo una sehemu za michezo, sehemu za mapumziko na maeneo ya usalama wa mji kama kituo cha polisi na zimamoto pamoja na maeneo ya wazi.
Kwa kipindi cha kuanzia Juni, 2022 hadi sasa, jumla ya viwanja 970 vyenye thamani ya Sh bilioni 19.64 vimeuzwa ambapo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekusanya Sh bilioni 12.33 sawa na asilimia 62.78 ya mauzo.
Pia, Shirika la Nyumba la Taifa tayari limejenga nyumba 10 za gharama nafuu za mfano, kuwawezesha wanunuzi wa viwanja takribani 23 kuanza ujenzi ambapo baadhi yao tayari wamehamia katika makazi yao.