Ujerumani yanasa vijana watatu kwa ugaidi

POLISI nchini Ujerumani wamewakamata vijana watatu kwa tuhuma za kupanga shambulizi la kigaidi.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka nchini humo wameeleza kwamba watuhumiwa hao ni wasichana wawili wenye umri wa miaka 15 na 16 na mvulana wa miaka 15.

Vijana hao watatu wametoka eneo la Dusseldorf katika jimbo la magharibi la Rhine-Westphalia na wanaaminika kuwa walikuwa wakipanga kufanya shambulio la kigaidi kwa kujiteketeza.

Ofisi Kuu ya Jimbo la Mashtaka ya Ugaidi ilitafuta hati ya kukamatwa kwa vijana hao wakati wa likizo ya Pasaka.

Mamlaka haikutoa maelezo zaidi kuhusu njama ya tukio hilo wala haikueleza jinsi mipango hiyo ilivyoendelea, ikitaja umri mdogo wa washukiwa na uchunguzi unaendelea.

Lakini gazeti la Bild liliripoti kwamba watu hao watatu wanadaiwa kupanga kufanya shambulizi dhidi ya waumini makanisani na kwenye vituo vya polisi kwa kutumia visu na vinywaji vya Molotov.

Mamlaka ya Ujerumani Januari iliwakamata watu watatu kwa madai ya njama ya kushambulia Kanisa kuu la Cologne katika mkesha wa mwaka mpya.

Pia mwezi uliopita, polisi waliwaweka kizuizini raia wawili wa Afghanistan wanaohusishwa na kundu la ISIL kwa madai ya kupanga kushambulia polisi karibu na bunge la Uswidi.

Hata hivyo taarifa zaidia zinaeleza kwamba ISIL pia wamekuwa wakitishia kushambulia viwanja vya soka kote Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ujerumani.

Mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya pia zilitishiwa na kundi hilo, lakini michuano hiyo iliendelea kama ilivyopangwa huko London, Paris na Madrid huku ulinzi mkali ukiimarishwa.

Habari Zifananazo

Back to top button