Ujumbe wa Mfuko wa Uwekezaji wa China na Afrika (CADFUND) unatarajiwa kufanya ziara nchini Tanzania mnamo Aprili, 2023.
Ahadi hiyo imetolewa jijini Beijing wakati Rais wa CADFUND, Song Lei alipokutana Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki.
Ujumbe huo utawasili nchini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa rai kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini wakati alipofanya ziara nchini China.
Mfuko wa CADFUND ulianzishwa na Serikali ya China kwa madhumuni ya kuwekeza Barani Afrika kwa ubia na makampuni ya China.
Mfuko huo wenye mtaji wa Dola za Kimarekani biliioni 10 umewekeza katika sekta za kilimo, uvuvi, madini, viwanda na mawasiliano.
Nchini Tanzania mfuko huo umewekeza katika miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa kiwanda cha kuzalisha saruji cha Maweni na mradi wa kilimo cha Katani mkoani Tanga.
Rais wa Mfuko huo Lei ameeleza kwamba kufuatia rai ya Rais wa Tanzania ya kukaribisha uwekezaji nchini pamoja na taarifa walizopata juu ya hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya awamu ya Sita za kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Mfuko wa CADFUND utakuwa tayari kuwekeza zaidi nchini Tanzania katika sekta za Kilimo, teknolojia na miundombinu.
Naye Balozi Mbelwa Kairuki ameahidi ameuhakikishia uongozi wa CADFUND kuwa utapata ushirikiano kutoka Serikali ya Tanzania kwa lengo la kufanikisha azma yao ya kuongeza uwekezaji nchini.