BARAZA la Madiwani wilayani Ukerewe, limepitisha bajeti ya Sh billion 4.4 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, huku utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha ukiwa umefikia asilimia 62.
Mwenyekiti wa halmashauri, Joshua Manumbu, amesema bajeti ya mwaka huu ni Sh billion 3.9, na ongezeko ni asilimia 11 (kutoka Sh3.9 hadi Sh billion 4.4), hatua itakayofanikisha ukamilishwaji wa miradi mbalimbali na hivyo kuwapatia wananchi huduma zote muhimu za kijamii.
“Tunakwenda kuimarisha ukusanyaji mapato hasa kupitia sekta ya uvuvi ili kukidhi matakwa ya bajeti hii tuliyopitisha,” alisema.
Amesema watahakikisha mianya ya upotevu wa mapato katika sekta ya uvuvi inazibwa kwa kasi wilayani humo, ikiwemo kudhibiti utoroshwaji wa mazao ya Ziwa Victoria, hasa samaki na dagaa, kwa kuimarisha doria ziwani.
Udhibiti huo unatokana na ukarabati wa boti mbili za mwendokasi ambao tayari umekamilika na boti hizo zitaanza kazi wakati wowote.
Pia halmashauri imetenga Sh millioni100 kwa ajili ya ujenzi wa boti mpya moja, na wakati huohuo Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh millioni 400 kwa Halmshauri za ujenzi wa boti zingine nne.
“Kwa hiyo tutakua na jumla ya boti saba. Hatua hii itasaidia kuimarisha doria kila sehemu ikizingatiwa kwamba asilimia 85 hadi 90 ya mapato tunaitegemea kutoka kwenye mazao ya uvuvi kwasababu wilaya yetu imezungukwa na maji,” amesistiza.