Ukiona changamoto siku ya sensa, piga simu hii

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amefanya ubunifu wa kuzindua namba ya dharura kwa wananchi wa mkoa huo ili kupiga na kutoa taarifa ya changamoto mbalimbali wakati wa sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu.

Akizungumza baada ya kukagua mafunzo ya makarani katika kituo cha Buigiri katika Shule ya Sekondari Chamwino wilayani Chamwino, Senyamule alitaja namba hiyo ya bure kuwa ni 0800110083.

“Mkoa wa Dodoma umezindua namba ya bure 0800110083 kwa ajili ya wananchi kutoa taarifa ya changamoto wakati wa sensa kama makarani watashindwa kutekeleza wajibu wao,” alisema.

Advertisement

Senyamule alisema kupitia namba hiyo ya bure wananchi wanaruhusiwa kupiga na kwamba ofisi ya mkuu wa mkoa itapokea taarifa za changamoto hizo na kutoa mrejesho mara moja kwa mratibu wa sensa mkoa na wilaya kwa ajili ya kufuatilia na kutatua.

Agosti 21 na 22, mwaka huu, makarani watapita na viongozi wa mitaa au vitongoji kuoneshana mipaka na kutambulishana kwa wanakaya sambamba na kutoa ratiba muda gani watapita kuhesabu watu waliolala siku ya sensa ili kaya hiyo ijipange kuwangoja siku hiyo.

“Kama makarani watashindwa kutekeleza ahadi ya kupita kama walivyoahidi, basi mwanakaya husika anaweza kupiga simu namba 0800110083 na kueleza changamoto hiyo katika ofisi ya mkuu wa mkoa ili ijue changamoto na kuitafutia ufumbuzi wake,” alisema.

Mkuu wa mkoa alipiga simu hiyo akiwa ukumbini katika Shule ya Sekondari ya Chamwino na kuzungumza na mwananchi, akahakikisha kwamba simu hiyo inafanya kazi vizuri na hivyo wananchi watumie fursa ya kupiga simu hiyo pindi wanapopata changamoto wakati wa kuhesabiwa.

Aliwataka viongozi mbalimbali katika ngazi za wilaya na halmashauri kusambaza namba hiyo kwa wananchi ili waijue na kuitumia kama wakipata changamoto wakati makarani wanapita kuhesabu watu. Senyamule alitumia wasaa huo kuwapongeza makarani wa wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla kwa kupata mafunzo ya siku 19 ambayo jana yalifungwa.

Akawataka wakatende kazi ya kuhesabu watu kwa uaminifu, uadilifu na uzalendo kwani taifa limeweka imani kwao.

/* */