Ukitupa hovyo taka Singida faini Sh 50,000

MANISPAA ya Singida imetakiwa kubadilisha mfumo wa kukusanya na kuhifadhi taka kwa kutunga sheria ndogo ambazo pamoja na mambo mengine, itawezesha atakayekamatwa akitupa taka hovyo kutozwa faini ya Sh 50,000.

Agizo hilo limetolewa Januari 20, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, baada ya kukagua maguba ya Kindai, Akwa, Uwanja wa Ndege na Kibaoni sokoni.

Serukamba pia amezuia utupaji wa takataka mitaani, badala yake kila mtu ahifadhi takataka anazozalisha nyumbani au sehemu yake ya kazi na azitoe kwa mzabuni atakayekuwa ameingia mkataba na manispaa hiyo, mara mbili kila wiki.

“Mtu akiwa na taka au asiwe nazo atalazimika kumlipa mzabuni kiasi cha fedha kilichoidhinishwa na manispaa,” amesema Serukamba.

Pia ameagiza vizimba vyote vinavyotumiwa kukusanyia takataka vivunjwe, maeneo hayo ipandwe miti na kulindwe na mgambo ambao watakamata kila atakayetupa takataka hapo na atatozwa faini ya Sh. 50,000 ambayo asilimia 50 yake itatumiwa kulipa  mgambo aliyemkamata.

Amesema takataka zote zitakazokusanywa na wazabuni, imeelekezwa zipelekwe moja kwa moja kwenye Dampo la Mwankoko.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili, amesema mpango wao ni kukuanya Sh. Mil. 30 kila mwezi, kutokana na tozo za taka ingawa mpaka sasa kiasi kinachokusanywa ni Sh Mil. 16, kiasi ambacho kimeongezeka kutoka Sh Mil. 3 zilizokuwa zikikusanywa awali.

Ofisa Mazingira wa Mkoa huo, Theresia John ametaja viwango vinavyotozwa sasa katika ukusanyaji taka kwenye Manispaa hiyo kuwa ni Sh 2000 kwenye makazi ya watu, kwenye biashara ni kati ya Sh 5,000 hadi Sh. 10,000 kwa mwezi, kutegemea na aina ya biashara.

Habari Zifananazo

Back to top button