UKRAINE imeadhimisha siku ya uhuru ikiwa ni miaka 31 tangu ijitenge na Umoja wa Kisovieti lakini pia ikiwa ni miezi sita tangu Taifa la Urusi lianzishe operesheni yake ya kijeshi nchini humo.
Gwaride la kijeshi lilijaa magari ya kijeshi ya Urusi yakihusisha vifaru vilivyotekwa ama kutelekezwa.
Sherehe hizo zimefanyika bila shamra shamra zilizozoeleka huku maafisa wakionya kuwa Urusi inaweza kufanya mashambulizi ya makombora dhidi ya miji ya Ukraine.
Ikumbukwe, sherehe hizi huhusisha gwaride maalum la kumbukumbu la hatua ambazo Ukraine ilipitia kujipatia Uhuru wake.
“Ukraine ilizaliwa upya Februari 24 saa 4 asubuhi. Tulikuwa ni taifa ambalo halikulia, halikupiga mayowe, halikuogopa. Wananchi hawakuikimbia nchi yao, hawakukata tamaa. Hawatasahau,” amesema Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy siku ya Jumatano akirejea uvamizi wa kijeshi wa Urusi.