TAIFA la Urusi limesema ndege mbili zisizo na rubani ‘Drones’ zimeshambulia Ikulu ya Kremlin mjini Moscow jana usiku katika tukio linalodhaniwa kuwa ni jaribio la Ukraine kutaka kumuua Rais wa taifa hilo, Vladimir Putin.
Taarifa ya Ikulu ya Kremlin imeeleza kuwa Putin hakuwa ikulu hapo hata hivyo hakukukuwa na uharibifu wowote na kwamba shambulio hilo lilizimwa na ulinzi wa Urusi.
Aidha taarifa ya Kremlin ilionya kwamba Urusi ina haki ya kulipiza kisasi na kwamba iliona shambulio hilo kama shambulio la “kigaidi”.
“Kremlin imetathmini vitendo hivi kama kitendo cha kigaidi kilichopangwa na jaribio la kumuua rais katika mkesha wa Siku ya Ushindi, Parade ya Mei 9,” chombo cha habari cha serikali RIA kiliripoti, na kuongeza Putin alikuwa hajabadilisha ratiba yake na alikuwa akifanya kazi kama kawaida.
Anton Gerashchenko, mshauri wa waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine, alisema wanaharakati wa Urusi wana uwezekano wa kuwa nyuma ya shambulio hilo, kwa mujibu wa Al-Jazeera.
“Habari zilionekana kuwa ndege isiyo na rubani huko Kremlin ilizinduliwa na wanaharakati wa Urusi kutoka Mkoa wa Moscow,” ameandika kwene kwenye Twitter.
Kremlin haikuwasilisha ushahidi wowote kutoka kwa tukio lililoripotiwa, na taarifa yake ilijumuisha maelezo machache.
Video ambayo haijathibitishwa inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii ya Urusi, ikiwa ni pamoja na chaneli ya chombo cha habari cha kijeshi Zvezda, ilionyesha moshi mweupe ukipanda nyuma ya Jumba kuu la Kremlin kwenye ngome iliyozungukwa na ukuta baada ya tukio hilo.