Ukweli ushirikiano uwekezaji bandari

WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi imetoa ufafanuzi wa mambo yanayopotoshwa au kutafsiriwa visivyo kuhusu makuabaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu uendeshaji na uendelezaji wa bandari.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mohammed Salum alitoa ufafanuzi huo juzi usiku katika mjadala wa wazi wa bandari kwenye Clubhouse uliosimamiwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.

Salum alisema Oktoba mwaka jana, Tanzania na Dubai zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika bandari lakini mikataba ya miradi bado haijasaniwa.

Alisema kampuni ya DP World si sehemu ya makubaliano ya Dubai na Tanzania, ila wametajwa na serikali ya nchi hiyo na kwamba Tanzania bado haijasaini mkataba na kampuni hiyo. “Emirates of Dubai wana uwezo wa kusaini mkataba huu kama taifa huru katika utekelezaji wa maeneo ambayo si Muungano wa nchi za Emirates (UAE),” alisema Salum.

Bandari haijauzwa Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Bandari ya Mwaka 2004 Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ni chombo pekee chenye mamlaka ya kumiliki bandari za Tanzania hivyo si kweli kuwa bandari zimebinafsishwa.

Salimu alisema kwa kuzingatia sheria hiyo hakuna chombo au mamlaka ya serikali yenye uwezo wa kuuza au kubinafsisha bandari za Tanzania.

“Sheria ya Bandari kifungu cha 5 na cha 12 kinaipa mamlaka TPA kukodisha maeneo ya bandari au kuingia mikataba na watoa huduma bandari katika maeneo ya bandari kwa ajili ya kuchagiza shughuli za bandari kuleta ufanisi,” alisema.

Aliongeza: “Bandari zitaendelea kumilikiwa na serikali na hakuna uuzaji wowote wa bandari, ni suala la kwenda kupangisha maeneo mahsusi ya bandari yaliyokubaliwa katika mkataba huo”.

Usalama wa nchi Salim alisema TPA ndiye mwenye jukumu la kuendesha bandari na si mwekezaji hivyo nchi itaendelea kuwa salama kwa kuwa mkataba wa nchi mwenyeji utaweka utaratibu wa majukumu kwa ajili ya usalama.

“Utekelezaji wa miradi hautaathiri usalama wa taifa letu…tulikuwa na TICTS (kampuni ya kimataifa ya huduma za makontena) kwa zaidi ya miaka 22 hatujawahi kupata tukio la usalama, na eneo la bandari pale kuna mkoa wa kipolisi kabisa na vyombo vyote, taasisi zote zinazopaswa kufanya kazi bandarini zitaendelea kufanya kazi zake kama ilivyo sasa hivi,” alisema.

Maeneo ya uwekezaji Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 5 (1) makubaliano hayo awamu ya kwanza itahusu baadhi ya maeneo ya Bandari ya Dar es Salaam pekee, maeneo mahsusi katika bandari kavu ya Kwala mkoani Pwani, eneo la Mamlaka ya Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA) Kurasini jijini humo.

Salum alisema ushirikiano huo pia utahusu kuiwezesha TPA kupata mifumo ya kisasa kuendesha bandari, kusaidia mafunzo katika vyuo, kuboresha magati ya abiria na majahazi ya yatakayoendeshwa na TPA.

Alitaja maeneo yatakayowekezwa kupitia mikataba mahsusi ya upangishaji wa miradi ni magati namba 1 hadi 7 na kwamba magati namba 8 hadi 11 hayamo katika makubaliano hayo sanjari na pia magati ya mafuta hayatahusika.

Kusitishwa, kuvunjwa mkataba Kwa mujibu wa Salum pia si kweli kwamba mkataba na mwekezaji hauwezi kuvunjwa. Alisema kwa kuzingatia maslahi ya nchi kifungu cha 14 cha makubaliano kinaipa serikali mamlaka ya kutaifisha mradi husika.

Salum alisema pia makubaliano hayo yametoa haki ya kusitisha mkataba iwapo nchi itaungana na nyingine au kuondoka ndani ya muungano na kusema katika hilo kumewekwa njia za utatuzi wa migogoro kwa njia za kidiplomasia ndani ya siku 90.

Alisema iwapo upande mmoja utashindwa unaweza kwenda hatua nyingine ya utatuzi wa migororo kwenye taasisi za kimataifa. Salum alisema pia si kweli kwamba mkataba hauwezi kuvunjwa na kwamba, kifungu cha 23 (3) kinaruhusu kuvunjwa na upande wa pili haupaswi kukataa bila sababu za msingi.

“Sisi tunaamini huwezi kuwa na mkataba ukaamka asubuhi ukasema mimi navunja mkataba, hata ukiwa na mpangaji wako huwezi kumfukuza tu bila kuwepo na mgogoro, huenda hajalipa kodi au mmeshatofautiana kuhusu matunzo ya nyumba, ndio unafikia hatua na kusema unavunja mkataba, ndio hivyo pia kwenye mkataba huo,” alisema Salum.

Mabadiliko ya mkataba Alisema kifungu cha 22 kinasema muda wowote unaweza kufanya mabadiliko ya mkataba kwa pande kukubaliana. Katika hilo Salum alisema upande mmoja wa mkataba ukiona kuna jambo haliko sawa katika mkataba unaweza kuomba kufanya mabadiliko.

Uhai wa mkataba Salum alisema uhai wa mkataba kati ya mwekezaji na TPA utazingatia muda wa makubaliano katika maeneo mahsusi baina ya pande hizo na bado haijasainiwa hivyo kusema ni wa milele huo ni upotoshaji.

“Akisema anawekeza kiasi kikubwa lazima utoe muda wa yeye kurudisha uwekezaji wake, hivyo bado hawajakaa kujadili hilo, serikali ikishakaa na DP World na TPA ndio tutajua na kuuweka kwenye mitakaba na miradi na huo ndio utakuwa muda wa mradi,” alisema Salum. Aliongeza: “DP World bado hawajafika nchini wala hawapo bandarini, kwa sababu hakuna mkataba wa mradi wowote kuhusu bandari ulioingiwa hadi sasa, tusipotoshe wananchi, muda ukifika serikali itasema”.

Mkataba na serikali, TPA Alisema kabla ya kusainiwa mikataba ya miradi wekezaji anapaswa kuwasilisha serikalini wasilisho la maeneo anapodhamiria kuwekeza na lilikubaliwa utasainiwa mkataba wa nchi mwenyeji utakaeleza utaratibu wa uwekezaji husika yakiwamo masuala ya kodi na mapato kwa ujumla.

Alisema baada kusainiwa kwa mkataba huo itasainiwa mikataba ya utekelezaji wa miradi husika na kwa maeneo ya mahsusi pia itasainiwa mikataba ya upangishaji itakayohusu ukubwa wa eneo husika na gharama za kupangisha.

Salum alisema baada ya hapo utafuata mkataba wa uendeshaji utakaohusu pia masuala ya tozo kwa kila kontena au mzigo anaohudumia kwa kila tani hivyo mwekezaji atakuwa na mikataba miwili na TPA.

Alisema katika mikataba hiyo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itakusanya kodi ya forodha kwa kila mzigo kwa mujibu wa sheria ya kodi ya forodha na akabainisha kuwa asilimia 90 ya mapato ya bandari yanakusanywa na mamlaka hiyo.

Salum alisema kwa mujibu wa kifungu cha 18 (1) cha makubaliano hayo kodi, ushuru na tozo vitatozwa kwa kuzingatia mifumo na sheria za Tanzania na motisha yoyote itatolewa kwa kuzingatia masharti ya sheria za Tanzania hivyo si kweli kuwa nchi itapoteza mapato.

Salum alisema kuhusu hoja ya kwamba TPA itaitaarifu Dubai kuhusu fursa nyingine alisema jambo hilo si la lazima. Hati ya kipekee Alisema pia si kweli kwamba serikali imetoa hati ya kipekee ya uwekezaji katika bandari, ila kilichofanyika ni kutoa miezi 12 tangu kusainiwa kwa makubaliano Oktoba mwaka jana kupisha majadiliano ya ushirikiano katika awamu ya kwanza.

Salum alisema kifungu cha 16 cha makubaliano kinaeleza kuwa viwango vya kiufundi vitazingatiwa katika utekelezaji wa miradi na si kweli kwamba serikali imetoa ridhaa zote kwa mwekezaji na ukweli ni kuwa zitatolewa kwa mujibu wa sheria na taratibu za Tanzania vikiwamo vibali.

Ardhi, motisha Pia alisema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa ushirikiano hakuna mwanachi atakayeguswa au kunyang’anywa ardhi kupitisha uwekezaji huo kwa kuwa utahusu maeneo ya bandari yanayomilikwa na TPA.

Salum alisema kama mikataba itasainiwa mwekezaji huyo atapewa motisha za uwekezaji kwa kuzingatia sheria na taratibu za Tanzania.

Pia alisema mwekezaji atapaswa kuhakikisha watumishi wote wanaofanya kazi bandarini wanaendelea kubaki kazini, iwapo itaajiri lazima aajiri Watanzania na iwape mafunzo na kuwaendeleza katika utekelezaji wa mradi husika.

Salim alisema atapaswa kuhakikisha zabuni za vifaa, huduma zinapewa kipaumbele kwa kampuni za ndani.

Habari Zifananazo

Back to top button