Ulaji kitimoto, ajali za bodaboda chanzo cha kifafa

Ulaji kitimoto, ajali za bodaboda chanzo cha kifafa

ULAJI wa nyama za nguruwe  (kitimoto) na ajali za barabarani zimetajwa kuwa sababu za ugonjwa wa kifafa kwa kundi la vijana nchini.

Sababu zingine zilizoainishwa uzazi pingamizi, upungufu wa kinga na homa kipindi cha utotoni.

Akizungumza leo  jijini Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya kifafa Duniani kila wiki ya pili ya mwezi Februari, mwakilishi wa Chama cha Wataalamu wa Ugonjwa wa Kifafa (TEA), Dk. Patience Njenje, amesema vijana wengine wanapata kifafa kwa sababu walipata tatizo wakiwa watoto, hivyo wanapofikisha miaka 15 kifafa kinaanza.

Advertisement

“Ajali za bodaboda zinaongoza kupata wagonjwa wa kifafa, utakuta mtu amepata ajali akapata matibabu vizuri na kuonekana amepona, lakini baada ya miaka mitano anaanza kuanguka kifafa na ulaji wa kitimoto ambacho hakijaiva vizuri,”ameeleza.

Pia Dk Njenje ametaja unyanyapaa na imani potofu kuwa ni changamoto kubwa, huku asilimia 36 ya watu wakiamini kifafa ni kurogwa.

Amesema asilimia 50 wanaamini kuwa mtu akivuta hewa ya mtu mwenye kifafa anapata na yeye kitu ambacho sio kweli.

Amebainisha kuwa hali hiyo ya unyanyapaa na imani potofu, inaathiri watoto kwani asilimia 45 hawapelekwi shule, asilimia 68 mahudhurio hayaridhishi huku watu wengine wakiwakataza watoto wao kucheza na mtoto mwenye kifafa kwa madai ya kuambukizwa.

“Wapo wanaoficha watoto ndani na asilimia 75 ya wagonjwa wanapelekwa kwa waganga wa kienyeji au kuombewa kwa viongozi wa dini na baada ya kuathirika asilimia tano hadi 10 hupelekwa hospitali, hivyo kwa sababu ya imani potofu tiba imekuwa ngumu,” amesema.

Dk Njenje amesema watu wanaoishi na kifafa ni zaidi ya milioni 60 duniani na katika kila watu 200,000 kuna ongezeko la watu 34 hadi 76 kwa mwaka.

Amesema Afrika ina idadi kubwa ya watu ambapo kati ya watu 1000 ni watu 10 hadi 50 wanapata.