Ulaji usiofaa, vilevi chanzo upungufu nguvu za kiume

PWEZA ni moja ya samaki wanaopatikana baharini lakini pia mwenye uwezo wa kuishi nchi kavu ambaye amepata umaarufu mitaani kutokana na manufaa yake katika mwili wa binadamu hususani kuongeza nguvu za kiume, madini na vitamini.

Wataalamu wa afya na lishe wanabainisha kuwa pweza ana zaidi ya virutubisho 12 vinavyopatikana kwenye supu au minofu ya samaki huyo ikiwamo protini, vitamini, selenium, madini ya chuma na zinki.

Kiuhalisia samaki huyu hana umbo la kutamaniwa kuliwa lakini wengi wakimuona pweza hupata kinyaa na kushindwa kumla, kutokana na mwonekano wa umbo lake wa kuwa na kiwiliwili kidogo na mikia mingi kama kichane cha ndizi.

Manufaa mbalimbali ambayo yanatokana na samaki huyo yamethibitishwa na tafiti za kitabibu na lishe. Hivi karibuni, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamiaji shughuli za lishe, Rais Samia Suluhu Hassan alibaini tatizo hilo na kuagiza kufanyika utafiti wa kwanini vijana balehe wana matatizo ya lishe ili kuepuka kuwa na taifa goigoi ambao ni mzigo kwa taifa.

“Watafiti fanyeni tafiti, tuna tatizo, kwa sababu halisemwi ni siri linawaumiza zaidi vijana wetu, mara vumbi la Kongo, mara supu ya pweza lakini tatizo kubwa liko kwenye lishe. Sasa watafiti fanyeni tafiti vijana wetu waweze kuzaa watoto wenye afya,” alisema Rais Samia.

Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Walbert Mgeni anasema ni kweli pweza ana virutubisho ambavyo vinachochea kuongeza nguvu za kiume, kuongeza maziwa kwa wanawake wakati wa unyonyeshaji na kuongeza madini joto mwilini.

Mgeni anasema kula pweza pekee si sababu ya kuongeza nguvu za kiume badala yake ili mwanaume apate nguvu hizo anahitaji kuzingatia ulaji unaofaa kutoka katika makundi matano ya chakula ikiwemo vyakula vyenye protini, wanga na vitamini mbalimbali ambazo hazipatikani kwenye pweza.

Anasema virutubishi vinavyopatikana kwenye vyakula ikiwemo vya asili ndivyo husaidia kutengeneza mbegu za kiume hivyo kutokula katika mpangilio inasababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari, shinikizo la damu ambalo husababisha kupungua kwa nguvu za kiume kwa watu wengi.

“Ili kuboresha afya ya uzazi kwa wanawake na wanaume, lazima kuzingatia lishe bora. Pweza ipo katika kundi la vyakula vya asili ya wanyama ambavyo vina protini inayojenga mwili, pia ana vitamini na madini ya zinki ambayo yanahusika moja kwa moja na nguvu za kiume,” anaeleza Mgeni.

Pia anasema kuwa masuala ya uzazi hayategemei kitu kimoja hivyo ni muhimu kila mtu kula vyakula vyenye kuwapatia nguvu, protini, matunda na mbogamboga kwa wingi na kuachana na matumizi ya vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi na sukari.

“Pweza ni chakula kizuri na mtu yeyote anaweza kula ili kuimarisha afya ya uzazi. Lakini kumekuwa na tabia ambayo si nzuri kwa baadhi ya wafanyabiashara kwa jinsi ambavyo pweza anatajwa kuongeza nguvu za kiume huchukua fursa hiyo kuongezea na dawa ikiwemo viagra jambo ambalo si salama kwa watumiaji wengine ambao wanatumia kitoweo hicho kama chakula kingine,” anasisitiza.

Anasema wapo baadhi ya vijana ambao wanakunywa vilevi vikali kwa kuchanganya wakiamini kwamba watakuwa vizuri, la hasha afya ya uzazi inahitaji nidhamu ili kufurahia tendo hilo na kupata kizazi bora.

Daktari wa Magonjwa ya Binadamu, Boaz Mkumbo anasema kuwa upungufu wa nguvu za kiume ni kitendo cha mwanaume kushindwa kupata hisia za kushiriki tendo la ndoa na mwanamke anayempenda huku wakiwa wameridhia.

Pia anasema kuwa sababu nne zinazochangia mwanaume kupunguza hisia ni kupata magonjwa yanayopandisha homoni ya prolactin katika damu na kuathiri maumbile ya kiume na hisia.

“Sababu nyingine ni magonjwa yanayochosha mwili kama vile kisukari, uzito uliokithiri, upungufu wa vitamini na madini, kukosa kujiamini, kujilinganisha maumbile na watu wanaocheza video za ngono za kulipwa na matumizi ya dawa za kulevya,” anasema Dk Mkumbo ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Nsambo Healthcare Polyclinic.

Anafafanua kuwa pweza ni samaki ambao ni chanzo kizuri cha virutubisho vya mwili kama Vitamin B6 na B12 na chanzo cha madini kama zinki na selenium ambavyo huondoa sumu na husaidia nevu za fahamu zifanye kazi vizuri.

Dk Mkumbo anasema pweza ni chanzo kizuri cha protini ya kujenga misuli na viungo vya mwili kwani huimarisha afya ya uzazi ya mwanaume hivyo ili wapate tiba na faida ya kula pweza wanatakiwa kula samaki, kuku, nyama, mayai kwa asilimia 75 na asilimia 25 iwe matunda, korosho, karanga lozi, mboga za majani na maziwa.

“Homoni za mwanaume zinaweza kuwa ziko vizuri katika kiwango toshelevu kabisa lakini mwanaume akiwa na magonjwa yanayochosha mwili kama kitambi, kisukari, shinikizo la damu huathiri hisia za mwanaume kwa kiwango kikubwa, hivyo dawa zote za mitishamba na za kizungu zitakuwa si suluhisho la kudumu,” anaeleza.

Anasema wengi wanaokula supu ya pweza pamoja na vyakula vya mafuta ikiwemo chapati huathiri mishipa ya damu kusukuma damu vizuri na kukupa hamasa kihisia.

Dk Mkumbo anaeleza kuwa mwanaume anaweza kugundua kuwa na upungufu wa nguvu za kiume pindi anapotaka kushiriki tendo la ndoa, magonjwa ambayo huathiri homoni za uzazi hivyo wanapaswa kufanya uchunguzi kwa njia ya damu ili kubaini upungufu wa madini na vitamini ambazo huratibu kasi ya shughuli za mwili.

Anasema ni vyema mtu mwenye tatizo hilo kuzungumza na madaktari ili kupata ufumbuzi na si kutafuta majibu kupitia mitandao au kwa watu ambao sio wataalamu na endapo mtu ameathirika kisaikolojia anapaswa aongee na daktari kuondoa hofu na kurudisha uwezo wa kujiamini.

Pia anasema wanaume wenye umri chini ya miaka 35 wengi wao wamejiathiri kisaikolojia kutokana na kujichua kwa kutumia video na picha za ngono, kutumia dawa za kemikali za kuongeza hisia ili kutumia muda mrefu na kulazimisha kuunganisha tendo la ndoa bila kupumzika baada ya kufikia kilele cha mapenzi (orgasm).

“Wanaume zaidi ya miaka 35 wengi wao unakuta wameathirika na maradhi kama kitambi, kisukari, shinikizo la damu, mwili kuwa katika msongo wa sumu za vyakula, magonjwa ya homoni ambayo hupunguza hisia kwa kasi.

“Matumizi ya pombe kupindukia, vimiminika vyenye sukari kama soda na juisi (sharubati), vyakula vya kukaanga kwenye mafuta mengi ya mbegu za mimea, sumu zitokanazo na mafuta, huathiri mishipa kutengeneza nitric oxide na kupunguza kiwango cha mzunguko wa damu katika mwili hivyo huathiri wingi wa damu inayohitajika ili mwanaume awe na hisia vizuri,” anasema Dk Mkumbo.

Anasisitiza kuwa changamoto nyingine ni magonjwa ya lishe, uvutaji wa sigara na dawa za kulevya huathiri homoni za uzazi na mishipa ya damu inayo sambaza damu vizuri ili mwanaume apate msisimko kihisia, msongo wa mawazo na kukosa muda wa kupumzika.

Dk Moses Manase anasema kuwa dawa za mitishamba na mimea mingine zimekuwa zikitumika tangu zamani hususani kwa wafalme waliokuwa na wake wengi hivyo ulaji wa pweza husaidia kwa kiasi mwanaume kuongeza hisia za tendo la ndoa.

Anaeleza kuwa wapo watu ambao wanarithi tatizo la nguvu za kiume kutoka kwa familia zao na wengine husababishwa na lishe na magonjwa sugu ikiwemo kisukari, shinikizo la damu ambayo huathiri hisia zao.

“Vijana waache kuangalia picha na video za ngono kwani jambo hili husababisha kushindwa kupata hisia hivyo kujiathiri kisaikolojia. Wenye matatizo wanapaswa kuwaona madaktari ili wawaeleze ni njia gani watumie kuepuka madhara makubwa,” anasema Dk Manase.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x