Ulega ang’oa uongozi mnadani Pugu

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Daniel Mushi kuuondoa uongozi wote wa Mnada wa Pugu mkoani Dar es Salaam kwa kushindwa kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato.

Ulega ametoa maelekezo hayo alipofanya ziara katika mnada huo uliopo wilayani Ilala jana, kwa lengo la kukagua na kubaini changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika mnada huo.

“Naibu Katibu Mkuu ondoa uongozi mzima wa hapa mnadani, kuanzia Msimamizi Mkuu na wengine wote, leta watu wengine na hao wengine utakaowaleta uwape miezi sita kisha uniletee taarifa kama wanakidhi viwango,” ameagiza Ulega.

“Nilileta timu hapa mwezi Desemba ikafanya kazi ya kukusanya mapato katika mnada huu, ndani ya siku 11 walikusanya zaidi ya Sh milioni 100, na hii inaonesha katika mnada huu mapato ni makubwa ila kuna baadhi ya watu wanajinufaisha,” ameongeza.

Aidha, amemuagiza Naibu Katibu Mkuu kuhakikisha anakagua minada yote mikubwa juu ya utendaji wao, na achukue hatua pale panapostahiki ili kuboresha shughuli za sekta ya mifugo nchini.

Amemuelekeza pia kuhakikisha ndani ya wiki moja kunajengwa ukuta uliodondoka katika mnada huo pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ili kuboresha mazingira ya mnada huo maarufu.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Stesheni, Shukuru Mwinjuma alitaja changamoto ya wafanyabiashara wadogo kukamatwa na mifugo yao kwa madai sio halali wakati wanavyo vibali vyote.

 

Habari Zifananazo

Back to top button