Ulega atoa ahadi kwa Rais Samia

Ni ya kuongeza uzalishaji, ajira kwa vijana

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amemuhakikishia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Sekta za Mifugo na Uvuvi zinakwenda kuongeza uzalishaji, kutoa ajira na kuleta tija kwa taifa.

Waziri Ulega amesema hayo leo mara baada ya kukabidhiwa ofisi na Waziri aliyemaliza muda wake Mashimba Ndaki kwenye Ofisi za Wizara zilizopo kwenye Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Amesema kuwa zipo fursa nyingi kupitia Sekta za Mifugo na Uvuvi ambazo zikitumiwa vizuri na vijana zinaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa kutoa ajira na kuongeza mchango wa sekta hizo kwenye pato la taifa. Hivyo amewasihi watumishi kufanya kazi kwa uweledi, ubunifu, uaminifu na kuongeza kasi katika utendaji.

Aidha, amewashukuru viongozi waliomaliza muda wao kwa ushirikiano ambao walimpatia wakati wote aliohudumu kama Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambapo pia amewasihi watumishi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi ili kufanikisha mikakati iliyowekwa ya kuendeleza sekta hizo.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde ameishukuru Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa ushirikiano waliompatia wakati akitekeleza majukumu yake lakini amewasihi watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na viongozi wote wapya ili kuhakikisha maendeleo kwenye sekta yanakua.

Silinde amesema ameletwa kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kushirikiana na viongozi waliopo kwa ajili ya kuhakikisha Wizara inatangazwa kutokana na kazi mbalimbali zinazofanywa ili wadau waweze kutumia fursa zilizopo kwenye Sekta za Mifugo na Uvuvi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amewasihi watumishi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Amewataka watumishi kutoa ushauri utakaosaidia kuzifanya Sekta za Mifugo na Uvuvi kuendelea kukua na kuzalisha kwa tija pamoja na kuwasihi watumishi kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na upendo.

Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo, Dkt. Daniel Mushi amesema kazi iliyopo ni kuhakikisha wanaendelea kusimamia utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa sekta ili uzalishaji wa mifugo na mazao yake unaleta tija kwa wafugaji na taifa kwa ujumla. Pia amesema Wizara itaendelea na jitihada ya kuimarisha taasisi zilizo chini yake ili kuhakikisha zinaendelea kutimiza wajibu wake katika kuleta maendeleo yanayotarajiwa.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Agness Meena amesema kuwa matarajio yake ni kuhakikisha kwanza wanasimamia utekelezaji wa mikakati ambayo tayari imeshawekwa na viongozi waliotangulia katika kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inakua.

Waziri aliyemaliza muda wake, Mashimba Ndaki amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpatia nafasi ya kusimamia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Vilevile amewashukuru watumishi wote kwa ushirikiano waliompatia wakati wa utekelezaji wa majukumu na ana imani kuwa ushirikiano huo utaendelea kutolewa kwa viongozi wapya.

Ndaki amewasihi viongozi kushirikiana na watumishi katika kutekeleza majukumu yao ili Sekta za Mifugo na Uvuvi ziweze kukua na kuongeza mchango wake kwa wafugaji, wavuvi na pato la taifa kwa ujumla.

 

Habari Zifananazo

Back to top button