NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema umefika wakati wataalamu wa mifugo kujengewa uwezo ili kutoa huduma zaidi maeneo ya vijijini na kulinda usalama wa mifugo na mlaji wa mazao yatokanayo na mifugo.
Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo Novemba 15,2022 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH) kwa wataalamu wa mifugo kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na baadhi kutoka nchi zingine duniani.
Amesema lengo la kuwakutanisha wataalamu hao ni kuwajengea uelewa wa pamoja na kupanga mikakati namna wanavyoweza kusaidiana na wataalamu wasaidizi kukuza sekta ya mifugo katika nchi zilizopo kwenye jumuiya hizo.
Aidha, amesema idadi ya madaktari na wataalamu wa mifugo waliopo nchini haitoshelezi kuenea maeneo yote ya nchi kwa kuwa sekta ya mifugo ni moja ya sekta kubwa hivyo lazima kuwe na mbinu mbadala za kuweza kuwasaidia wafugaji kuhakikisha mifugo yao haipati maradhi wala kufa kwa magonjwa.
Wafugaji wengi wapo vijijini kwa idadi ya madaktari au wataalamu wa mifugo tulionao haitoshelezi kusema wataenea kote, tunao kama 5,600 kote nchini ukilinganisha na ukubwa wa sekta ni wakati wa kuweka mikakati namna ambavyo tunaweza kuwasaidia kufika hadi vijijini.
”
Kwa upande wa msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) Dkt. Amani Kilemile amesema majukumu waliyonayo ni kuhakikisha huduma za matibabu ya mifugo zina kuwa bora kwa kufuata sheria zilizoanzisha baraza hilo kwa kusimamia pia ubora wa elimu kwa wataalamu wa mifugo kuanzia ngazi ya cheti.m
Amesema baraza linahakikisha linawatambua wataalamu wa mifugo ambao wamesajiliwa kupitia baraza hilo pamoja na kufuatilia mienendo yao ukiwemo utendaji wao wa kazi katika kuhudumia mifugo kwa njia sahihi inayokubalika kitaalamu.
Kongamano hilo linalowahusisha wataalamu wa mifugo kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na baadhi kutoka nchi zingine duniani, lililoandaliwa na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH) linalenga kubadilishana kwa uzoefu wataalamu wa mifugo katika njia ya utendaji kazi na kuweka mikakati ya namna ya kuboresha sekta ya mifugo katika nchi zilizopo kwenye jumuiya hizo.