MWANZA: JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limeimarisha ulinzi maeneo yote ya nchi kavu na majini katika Ziwa Viktoria kwa kuongeza doria na misako kuelekea sikukuu ya Mwaka Mpya, 2024.
Kauli hiyo imetolewa leo Disemba 30, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa wakati akitoa elimu kwa umma kupitia chombo kimojawapo cha habati kilichopo Jijini Mwanza.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeongeza askari maeneo yote yakiwemo ya miradi ya kimkakati ya Serikali ili kudhibiti wizi na uhalifu wowote utakaojitokeza,” amesema SACP Mutafungwa.
“Sisi Jeshi la Polisi hatupo likizo, tupo imara na tupo kazini muda wote, tumejipanga imara kwa kushirikisha Jeshi la Akiba (Mgambo) ili kudhibiti maeneo yote ya kumbi za starehe, sehemu zenye mikusanyiko, sehemu za ibada na barabarani,” Amesisitiza Kamanda huyo.
Akijibu swali la mtangazaji katika kipindi hicho, kuhusu kutunza siri za watoa taarifa za uhalifu kwa Jeshi la Polisi, Kamanda Mutafungwa amewatoa hofu wananchi na amewataka wasipoteze imani na Jeshi lao kwani hata mafanikio ya kuzuia uhalifu yaliyopatikana yametokana na taarifa za wananchi.
“Tumefanikiwa kuzuia mauaji ya imani za kishirikina kwa kutoa elimu kwa waganga wa tiba asilia ambao wamekuwa wakitupatia taarifa za waganga wasio waaminifu pamoja na wahalifu na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.” Asema Kamanda Mutafungwa.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa ameendelea kutoa onyo kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani. Kwamba Jeshi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa madereva wasiozingatia sheria.